Habari Mseto

Wanawake watatu washtakiwa kuweka pilipili kwenye sehemu za siri za mwenzao

Na TITUS OMINDEĀ  October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WANAWAKE watatu wameshtakiwa kwa madai ya kuweka pilipili kwenye sehemu za siri za mwanamke mwingine wakimlaumu kwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na waume zao.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 24 aliripotiwa kushambuliwa na watatu hao ambao walimshtumu kwa kunyakua waume zao.

Kulingana na polisi, kisa hicho kilitokea Kapseret kaunti ya Uasin Gishu mnamo Oktoba 1.

Mwathiriwa aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Kapseret.

Walioshuhudia tukio hilo walidai kuwa wanawake hao waliokuwa na hasira walimrai mwathiriwa hadi nyumbani kwa mmoja wao ambapo walimvua nguo huku na kuweka pilipili kwenye sehemu zake za siri.

“Tulisikia mwathiriwa akipiga kelele kutoka kwa nyumba ambayo tukio lilitokea, tulipoenda huko tulimkuta akiomba washukiwa wamsamehe, baadaye tuliingilia kati na kumshauri aende hospitali asaidiwe,” alisema mmoja wa walioshuhudia.

Washukiwa pia walimshambulia mwathiriwa kwa kumdhuru mwilini.

Mwathiriwa, ambaye alikuwa na alama za mateso kwenye mwili wake alitibiwa katika hospitali moja ya eneo hilo.

Polisi baadaye waliwakamata washukiwa na kuwaafikisha katika mahakama ya Eldoret mnamo Jumanne.

Washukiwa hao walitambuliwa kama Monicah Jeptum, Joyce Jerobon na Caroline Jerotich.

Walishtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia kinyume na makosa ya ngono ya 2007.

Vile vile walishtakiwa kwa kushambulia na kumjeruhi mwathiriwa.

Walikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Eldoret, Mogire Onkoba na wakaachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh100,000.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 4.