Lugha, Fasihi na Elimu

NDIVYO SIVYO: Miktadha inayotofautisha matumizi ya neno ‘kasri’

Na ENOCK NYARIKI October 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MIONGONI mwa mijadala ambayo imekuwa ikijirudiarudia kwenye majukwaa kadha ya usanifishaji wa lugha ni kuhusu ngeli na upatanisho wa kisarufi wa baadhi ya nomino.

Yamkini kutokana na maumbo ya maneno mengine, watumizi wa lugha ya Kiswahili huyachukulia kimakosa kwamba yanapaswa kuwa katika ngeli ya LI-YA hivyo basi yanapaswa kufuata upatanisho wa kisarufi wa ngeli hiyo. Mathalan, utawasikia wakisema ‘hoja la pili’ badala ya ‘hoja ya pili’.

Katika makala haya, nimepania kuliangazia neno ‘kasri’ na utata wa upatanisho wa kisarufi unaolizunguka neno lenyewe na maneno mengine yanayohusiana nalo. Mjadala wetu utazunguka vivumishi vya A-unganifu vinavyotumiwa pamoja na neno tulilolitaja.

Etimolojia ya neno ‘kasri’ ni Kiarabu. Maana ya asili kabisa ya neno hilo, na ambayo imepewa kipau mbele katika machapisho ya awali ya kamusi (Kamusi ya Kiswahili Sanifu na Kamusi ya Kiswahili- Kiingereza; TUKI) ni ile ya jumba la kifalme. Hii ndiyo maana ambayo neno hilo lilihusishwa nayo katika mazingira ya Kiarabu.

Aghalabu, maneno mengi ambayo asili yake ni ya kigeni, huingia kwa urahisi katika ngeli ya I-ZI. Kasri ni mfano mmojawapo wa maneno hayo.

Yeyote aliyelitumia neno hilo kuyarejelea makazi maalumu ya mfalme, aliliambatanisha na kivumishi cha A-unganifu ‘ya’.

Kadiri neno lenyewe lilivyokita mizizi kimatumizi, lilipokea maana ya ziada ambayo yamkini ilitokana na uhusishaji walo na jengo lolote kubwa na la kifahari hasa lililojengwa kwa ajili ya makazi.

Kwa kudumisha sifa hiyo ya ukubwa, watumizi wa lugha ya Kiswahili walibadilisha upatanisho wa kisarufi ukawa ‘kasri la’. Linalochangia mabadiliko ya A-unganifu ni muktadha wa matumzi.

…YATAENDELEA