Tambua kwa nini mshukiwa mkuu wa mauaji ya wanawake Nakuru amegeuka shahidi
MSHUKIWA mkuu katika kesi ya mauaji ya wanawake katika eneo la Mawanga kaunti ya Nakuru ameafikia makubaliano ya kukubali kutoa ushahidi dhidi ya washtakiwa wenzake watano.
Hii inafuatia makubaliano ya Evans Kebwaro Michori kujibu shtaka dogo la kuua bila kukusudia.
Wakili wa serikali James Kihara alimweleza Jaji Patricia Gichohi jana kwamba Kebwaro alikuwa amejutia makosa yake na kujitolea kwa hiari kuwa shahidi wa upande wa mashtaka.
Hatua hiyo ni sehemu ya maafikiano ya kesi nne za mauaji anazokabiliwa nazo pamoja na washukiwa wenzake.
Bw Kebwaro na wengine watano—Mabw Kevin Otieno, Josphat Juma, Julius Omondi, Dennis Mbolo, na Isaac Nganga—wanashtakiwa kwa mauaji manne katika Jiji la Nakuru yaliyotokea kati ya 2021 na 2022.
Walishtakiwa mnamo Agosti 2022 kwa mauaji ya Grace Wanjiru (20), Susan Wambui (38), Diana Opicho (23), na Beatrice Akinyi (21).
Mnamo Agosti 2022, Kebwaro alikana mauaji hayo lakini baadaye akaomba makubaliano, akiamua kukiri kosa la kuua bila kukusudia.
Upande wa mashtaka ulikubali na akakiri kuhusika kwake katika mauaji hayo yanayohusisha wenzake.
Shtaka lake jipya linamshtaki kwa kushiriki njama ya kuficha mwili wa Bi Opicho, aliyeuawa Juni 24, 2022, katika eneo la Mawanga, kaunti ndogo ya Bahati.
Akijitetea, Bw Kebwaro aliomba mahakama kumhurumiwa, akisema alishirikiana na polisi, ambapo ushirianano wake ulisababisha kukamatwa kwa washukiwa hao wengine.
Pia aliangazia kukiri kwake ambako alisema kuliokoa muda wa mahakama.