Kimataifa

Familia za wahamiaji Amerika zahofia Trump kurejea kama rais

Na MASHIRIKA October 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON D.C, AMERIKA

FAMILIA za wahamiaji zilizotenganishwa wakati wa utawala wa aliyekuwa rais Donald Trump, zingali zinahisi kutengwa huku zikihofia kurejea kwake mamlakani.

Maelfu ya watoto walitenganishwa na wazazi wao kwenye mpaka kati ya Amerika na Mexico kutokana na sera iliyopiga marufuku uhamiaji iliyoanzishwa na Trump alipokuwa akitawala kama rais wa 45.

Huku Amerika ikielekea uchaguzini hapo Novemba 5, uchaguzi ambao huenda ukamrejesha Trump mamlakani, wahasiriwa wengi wamefunguka mioyo kuhusu masaibu waliyopitia.

Baadhi ya familia zingali hazijaunganishwa na sehemu kubwa ya walio pamoja wana kibali cha muda na wanahofia ushindi wa Trump aliyeahidi kurejesha maelfu ya wahamiaji makwao.

“Ni jambo la uchungu mno tulilopitia,” anaeleza Billy, aliyechelea kutajwa akihofia kuhatarisha nafasi ya familia yake kupatiwa kibali cha kupatiwa hifadhi.

Alikuwa na umri wa miaka tisa alipotenganishwa na familia yake.

Trump ameweka msimamo kuhusu uhamiaji kama nguzo ya kampeni yake akishutumu serikali ya Rais Joe Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris, ambaye ni mgombeaji wa urais kwa chama cha Democratic, kwa kukosa kuimarisha ulinzi kwenye mpaka wa kusini.

Harris hajaangazia uhamiaji katika kampeni yake lakini amezungumzia kuhusu sera ya Trump ya kupiga marufuku wahamiaji, ambayo ni miongoni mwa hatua zenye utata zaidi alizochukua akiwa rais.

Utawala wa Trump ulinuia kuwashtaki watu wazima wote wanaovuka mpakani kimagendo.

Wazazi walitenganishwa na watoto wao waliohamishwa katika makazi ya kuwatunza watoto kote nchini.

Trump na kampeni yake hakusema waziwazi ikiwa atafufua mtindo huo endapo ataibuka mshindi Novemba 5, japo hapo awali ametetea msimamo huo.

“Rais Trump atarejesha sera zake thabiti kuhusu uhamiaji, atekeleze msako mpya utakaotikisa walanguzi wa uhalifu kimataifa na kukusanya kila uwezo unaohitajika nchini kuanzisha oparesheni kuu ya kuwarejesha makwao kimabavu wahalifu, walanguzi wa mihadarati na binadamu katika hitsoria ya Amerika,” alisema Karoline Leavitt, katibu wa kampeni ya Trump.

Harris aliandaa hafla mwezi huu iliyoshirikisha watoto waliotenganishwa na familia zao akikusudia kumulika sera za Trump.

Billy aliyezungumza katika hafla hiyo ni miongoi mwa watoto wanaosimulia masaibu yao kupitia video fupi kwenye mitandao ya kijamii kuangazia sera hiyo.

Anasema, “Tunahakikisha tunapaaza sauti zetu na kusimulia yaliyotupata,” ili jambo kama hili lisiwahi kamwe kutendeka tena.