Madaktari watoa kauli, wasema SHIF na SHA ni hadaa tupu
MADAKTARI na wahudumu wengine wa afya eneo la Pwani wamepinga vikali Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) wakitaka isimamishwe.
Chama cha madaktari (KMPDU) tawi la Pwani kimesema bima mpya inayoendeshwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) ni mbovu na kuwa madaktari na wagonjwa wanahangaika.
Wanasema bima hiyo imepingwa na vituo vya afya vilivyotia saini mkataba na SHA huku wagonjwa wakilazimika kulipia huduma pesa taslimu.
Hospitali hizi zimeendelea kukumbwa na matatizo ya kudai pesa kwenye tovuti ya SHIF licha ya hakikisho kutoka kwa Waziri wa Afya Deborah Barasa kuwa shida zimetatuliwa.
Akizungumza katika mkutano wa kila mwaka mnamo Jumamosi, Katibu wa KMPDU Dkt Ghalib Salim alitaja SHA na SHIF mradi unaofyonza pesa za umma bila kuwafaidi (white elephants).
“Tunawatibu wagonjwa lakini sisi hatuwezi kufikia huduma za tiba chini ya SHIF. Bima hii haifanyi kazi,” alifoka.
Alidokeza kuwa mfumo huo mpya unaathiri vibaya huduma muhimu ikiwa ni pamoja na tiba ya meno ya kila mwezi kwa Sh950, na kuweka ukomo wa tiba ya kuosha damu na saratani kuwa mara moja kwa mwezi.
Chini ya SHIF, wafanyakazi wote wanatarajiwa kuchangia asilimia 2.75 ya mishahara yao kwa hazina mpya ya afya.
Chini ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF), ambayo ilisitishwa, Wakenya walikatwa kati ya Sh150 hadi Sh1,700 kwa wafanyakazi wanaolipwa mishahara na Sh500 kwa wale wa kujiajiri.
Wakenya wanaopata mishahara ya Sh20,000 walikatwa Sh750, huku wanaopata Sh50,000 wakilipa Sh1,200.
Wanaopata Sh100,000 na zaidi walikatwa Sh1,700. Kikomo cha juu cha Sh1,700 kwa wale wanaopokea Sh100,000 au zaidi kitaondolewa.
Chini ya SHIF wanaopata Sh20,000 wanakatwa Sh550 huku Wakenya wanaopokea mshahara wa Sh50,000 wakilipa Sh1,375.
Wakenya wenye mishahara ya Sh100,000 wanakatwa Sh2,750 na wale wanaopata Sh200,000 wakilipa Sh5,500.
Kwa mishahara ya Sh500,000 wafanyakazi wanalipa Sh13,750 huku wale wa Sh1 milioni na zaidi wakilipa Sh27,500.
Kulingana na Mwenyekiti wa KMPDU Pwani, bima hiyo imewaacha wahudumu wa afya na umma katika hali mbaya.
“Kulikuwa na bima ya afya ya jumla kwa wafanyakazi waliotumwa kutoka Wizara ya Afya. Sasa, bila idhini inayofaa, wanachama wetu wanalazimika kujilipia,” Dkt Gichana alisema.
Alisema kati ya serikali za kaunti sita za Pwani, Kilifi na Taita Taveta pekee ndizo zilizotimiza makubaliano ya kuheshimu matakwa ya madaktari.
Madaktari wengi wanalilia kupandishwa vyeo kama inavyofaa wakiteta kuhusu kucheleweshwa kwa mishahara.
Hii ni licha ya maelewano ya kurejea kazini kutiwa saini Mei 8, kama wanavyoripoti maafisa wa chama hicho.
Viongozi hao kadhalika wameweka wazi masaibu ya madaktari walioajiriwa, ambao wengi wao wana matatizo ya kifedha kutokana na kucheleweshwa kwa mishahara tangu Agosti.
“Tulianza kufanya kazi Agosti 5, 2023. Leo ni Oktoba na hatujalipwa. Hatujui ni lini au kiasi gani tutalipwa,” alilalamika daktari mwanagenzi Collins Olondo.
Muungano huo umeonya kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kushughulikia malalamishi ya madaktari, mfumo wa huduma za afya nchini Kenya unaweza kusambaratika.
Imetafsiriwa na Labaaan Shabaan