Mshangao watahiniwa 23 wa KPSEA wakifanyishwa mtihani feki Eldoret
HATIMA ya watahiniwa 23 wa mtihani wa Gredi ya Sita (KPSEA) katika Kaunti ya Uasin Gishu haijulikani baada ya kubainika kwamba walikalia mtihani feki.
Shule hiyo, Silver Bells Academy eneo la Kimumu, Eldoret haikuwa imesajiliwa na Baraza la Mitihani ya Kitaifa, Knec.
Sasa imebainika kwamba ‘mitihani’ waliyokalia tangu Jumatatu kumbe ni karatasi za mwaka jana zilizotolewa fotokopi.
Kikosi cha maafisa wa Wizara ya Elimu na Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, kilivamia shule hiyo na kukamata wakurugenzi wawili wa shule hiyo.
Mtihani wa KPSEA umekamilika leo Jumatano ambapo watahiniwa zaidi ya milioni waliukalia kote nchini.