Hamtaiweza Man United tena, adai kocha mshikilizi Ruud Van Nistelrooy
MANCHESTER, UINGEREZA
KOCHA mshikilizi wa Manchester United, Ruud van Nistelrooy amesema klabu hiyo itakuwa kali zaidi, japo baada ya maandalizi makali.
Nistelrooy ambaye alichezea klabu hiyo pamoja na timu ya taifa ya Uholanzi atasimamia mechi ya Jumatano usiku dhidi ya Leicester City ugani Old Trafford katika gozi la Carabao Cup, raundi ya 16-bora.
“Ninaamini Manchester inaweza kurejea katika kiwango chake cha zamani nilichojua nikiwa mchezaji. Nina hiyo imani, lakini itachukua muda na bidii nyingi,” Van Nistelrooy alisema kabla ya timu hiyo kucheza na Leicester City.
Nyota huyo msataafu alipewa jukumu la kusimamia timu hiyo baada ya klabu hiyo kuagana na Erik ten Hag aliyeiacha katika nafasi ya 14 kutokana na matokeo duni.
Wakati Nistelrooy akihudumu kama kaimu kocha, wakuu wa klabu hiyo wanafanya mazungmzo na kocha Ruben Filipe Amorim kujaza nafasi hiyo.
Van Nistelrooy alichezea Manchester United kwa miaka mitano kuanzia 2001 hadi 2006, akiisaidia kushinda taji la EPL, FA Cup, EPL Cup na Community Shield. Alirejea msimu uliopita kama naibu wa Ten Hag.
Staa huyo mstaafu aliyekuwa kocha wa PSV Eindhoven kwa mwaka mmoja kuanzia 2022, anaamini atafaulu kama kaimu kocha kwa ushirikiano na wasaidizi wake.
Wakati huo huo, mshambuliaji Diogo Jota wa Liverpool atakaa nje kwa mwezi mmoja bila kucheza baada ya kuvunjika mbavu, kocha wake Arne Slot amethibitisha.
Mshambuliaji huyo raia wa Ureno aliumia Oktoba 20 baada ya kugongana na Tosin Adarabioyo wa Chelsea kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambayo klabu yake iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Tayari nyota huyo amekosa kucheza mechi mbili zilizopita na hajarejea mazoezini tangu apate jeraha hilo.
Kulingana na ripoti ya daktari, staa huyo mwenye umri wa miaka 27 atakosa mechi nne zijazo katika mashindano tofauti, zikiwemo za kimataifa zitakazochezwa kuanzia Novemba 11 hadi 19.
Mbali na Jota, Liverpool itawakosa kipa Alisson, Harvey Elliot na Federico Chiesa wanaotarajiwa kurejea baada ya wiki kadhaa.
Liverpool itakutana na Brighton katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itakayochezewa Anfield, Jumamosi.
Baadaye, kikosi hicho cha kocha Slot kitakaribisha Bayer Leverkusen katika pambano la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kisha kuvaana na Aston Villa kabla ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa.
Baada ya mapumziko hayo, mechi yao ya kwanza itakuwa dhidi ya Southampton Novemba 24.