Mwisho wa lami: Gachagua hatimaye aishiwa na maarifa
JUHUDI za Naibu Rais aliyetimuliwa ofisini Rigathi Gachagua kusimamisha kuapishwa kwa Prof Kithure Kindiki kama naibu rais mpya wa Kenya ziligonga mwamba Alhamisi.
Bw Gachagua alipata pigo mara mbili kortini, Mahakama ya Rufaa ilipokataa kusimamisha majaji watatu walioteuliwa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alivyotaka na Mahakama Kuu ikaondoa agizo la kuzuia mrithi wake kuapishwa.
Muda mfupi baada ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, Majaji watatu ambao Bw Gachagua alikuwa akipinga kusikiza kesi yake waliondoa agizo lililompa afueni kwa wiki mbili tangu atimuliwe na Bunge la Kitaifa na Rais Ruto akateua Profesa Kindiki kuwa naibu rais.
Majaji wa mahakama ya rufaa Patrick Kiage, Aggrey Muchelule na George Odunga waliagiza kesi iliyowasilishwa na Bw Gachagua isikizwe mnamo Novemba 6, 2024.
“Hatuwezi kutoa amri kwa wakati huu (ya kuzuia majaji wa Mahakama Kuu),” waliamua majaji. Bw Gachagua alifika Mahakama ya Rufaa wiki jana akitaka amri ya kutangaza jopo la majaji walioteuliwa na Jaji Mwilu kuwa kinyume na katiba.
Katika uamuzi wao, majaji wa Mahakama ya Rufaa walitaja kesi iliyoorodheshwa mbele ya majaji watatu waliokuwa wakisubiri kutoa uamuzi katika kesi ambapo Bw Gachagua alidai Prof Kindiki hakustahili kuteuliwa kuwa naibu rais.
Katika uamuzi wao, Majaji hao watatau wa Mahakama Kuu waliondoa agizo lililotolewa na Jaji Richard Mwongo wa Mahakama Kuu ya Kerugoya kuzuia kuapishwa kwa Profesa Kindiki kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na Bw Gchagua, kupinga kutimuliwa kwake.
Katika uamuzi wao, Majaji Anthony Mrima, Eric Ogola na Freda Mugambi walisema wadhifa wa naibu rais hauwezi kubaki wazi.
“Mahakama hii inabainisha kuwa afisi ya naibu rais haiwezi kubaki wazi na hivyo mahakama itakuwa upande wa Katiba ambayo inaeleza kuwa lazima wadhifa huo ujazwe,” majaji hao walisema.
Walibainisha kuwa kesi hiyo ina maslahi makubwa ya umma na walijitolea ‘kutoa uamuzi wa haraka kwa kesi kadhaa’ zilizokuwa mbele yao. Zaidi ya kesi 30 ziliwasilishwa kuzuia Bw Gachagua kuondolewa ofisini ambazo ziliunganishwa. Bunge la Seneti na Mwanasheria Mkuu walifika mbele ya majaji hao watatu wa Mahakama Kuu kutaka agizo la kuzuia kuapishwa kwa kindiki liondolewe.
“Maagizo ya muda yaliyotolewa Oktoba 18, Kerugoya yameondolewa,” waliamua majaji hao, na kuongeza kuwa Bw Gachagua na walalamishi wengine wako huru kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Bw Gachagua aliondolewa afisini Oktoba 17 naye Prof Kindiki akateuliwa na Rais William Ruto siku iliyofuata, na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa.
Bw Gachagua na walalamishi wengine, hata hivyo, walikimbilia kortini na kupata maagizo ya kuzuia kuapishwa kwa waziri huyo wa usalama wa ndani kusubiri uamuzi wa kesi.
Bw Gachagua aliteta kuwa alinyimwa haki ya kusikilizwa kwa haki na kwamba ushiriki wa umma ulioendeshwa na Bunge haukufikia kiwango cha kikatiba.
Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor, na Bunge la Seneti walipinga agizo ka kuzuia kuapishwa kwa Profesa Kindiki wakisema kuwa lilikuwa na athari kubwa ambazo zinaweza kuingiza nchi katika mzozo wa kikatiba.
Alhamisi, majaji wa Mahakama Kuu walikubaliana nao kwamba Katiba haitoi nafasi ya kuwepo kwa pengo katika ofisi ya naibu rais.
Bila agizo kutoka Mahakama ya Rufaa, mchakato wa kumuapisha Profesa Kindiki unaweza kuendelea.