Hujambo shangazi? Pamoja na mume wangu tumeoana kwa miaka 15 na tumejaliwa watoto watatu.
Hata hivyo, watoto hawa wote sio wake.
Tukichumbiana, mume wangu alikuwa mgonjwa sana na hapa ndipo daktari alinifichulia kwamba hakuwa na uwezo wa kutungisha mimba. Kwa sababu nilikuwa nampenda na alikuwa na mali, niliamua kuolewa naye lakini kila tulipotaka mtoto, nilikuwa nikilala na wanaume wengine. Nitamwambiaje ukweli hasa wakati huu ambapo yeye ni mgonjwa mahututi?
Jambo ulilofanya halifai lakini siwezi kukushauri umwambie ukweli hasa wakati huu. Kuna wakati mwingine ambapo ukweli lazima ufichwe ili kulinda usalama au afya ya mtu.
Nataka kuongeza ‘chuma’
Shikamoo shangazi? Kwa miaka mingi nimekuwa nikikabiliwa na hisia za kutofaa hasa inapowadia katika masuala ya mahaba. Kila ninapokutana na binti, pindi tu tunaposhiriki tendo la ndoa, natemwa. Sababu ni kuwa uume wangu ni mdogo sana. Nataka kufanyiwa upasuaji kuongeza sehemu hii.
Marahaba! Una uhakika upi kuhusu usalama wa utaratibu unaotaka kufanyiwa?
Pia, una uhakika upi kwamba baada ya hapo utaridhika mwenyewe?
Cha muhimu ni kujikubali jinsi ulivyo na usimruhusu yeyote kukufanya uhisi kana kwamba hufai.
Nampenda vivyo hivyo!
Mpendwa shangazi. Nilikutana na binti mmoja miezi kadhaa iliyopita na nampenda sana. Tatizo ni kuwa yeye ni mlemavu –ana nundu mgongoni. Tunapanga kuoana lakini familia yangu imekataa kabisa kumkubali na haitaki nimuoe. Nifanyeje?
Hongera kwa kufanya uamuzi wa kumpenda mwenzako pasipo kuangalia masuala ya kimaumbile. Pili, uhusiano wa mapenzi na hata ndoa ni uamuzi baina ya watu wawili. Bila shaka ni muhimu kusikiza ushauri kutoka kwa jamaa zako hasa kuhusiana na masuala mengine kumhusu mwenzako, na wala sio kwa misingi ya kimaumbile.