Makala

Hivi ndivyo Rigathi Gachagua alijiporomosha

Na KENNEDY KIMANTHI November 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA siasa za Kenya, mamlaka yanapasa kutumiwa kwa uangalifu kiongozi anapolenga kufikia malengo yake, funzo ambalo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alipitia kwa machungu.

Japo aliheshimiwa kama kiongozi mwenye mamlaka makubwa katika serikali ya Kenya Kwanza, alikosea kwa kutozingatia misingi ya mamlaka yaliyomo katika kitabu cha Robert Green, “The 48 Laws of Power”.

Kwa kujaribu kuonekana anampiku mkubwa wake na kukosana hadharani na wandani wa Rais, Gachagua alivunja kununi za kumwezesha kudumu katika ulingo wa siasa.

Kimsingi, Gachagua aliyepoteza nafasi hiyo Ijumaa kufuatia kuapishwa kwa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais, alikiuka sheria tatu kuhusu mamlaka.

Kila moja ya kanuni hizo ni kielelezo cha jinsi Gachagua alifeli.

Usishindane na mkuu wako

Kanuni ya kwanza yasema, Usidhubutu kumpiku mkubwa wako. Gachagua ambaye alihudumu kwa muhula mmoja kama mbunge wa Mathira, alionekana kuhisi kwamba yeye alikuwa Rais mwenza.

Hii ndiyo maana wakati mmoja Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar alionya wandani wa Bw Gachagua dhidi ya kuendeleza dhana hiyo.

Katika mikutano kadhaa ya hadhara na mahojiano kwenye vyombo vya habari, Bw Gachagua alisema ushindi wa Rais Ruto ulichangiwa pakubwa na kura za Mlima Kenya na kwamba yeye akiondolewa basi Rais pia anafaa kuondoka mamlakani.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Mark Situma, hatua ya Gachagua kujaribu kujijengea himaya ya kisiasa kivyake nje ya kivuli cha mkubwa wake, ndiyo ilimletea masaibu.

Ficha malengo yako

Kulingana na mwandishi Robert Green, kanuni nambari ya pili nayo yasema, ficha malengo yako. Waweke watu gizani kuhusu mipango yako. Usiende mpaka ukapita hatua uliyolenga.

Jua wakati wa kusita kwa muda. Bw Gachagua alikiuka kanuni hii kwa kuonyesha ndoto zake za kisiasa mapema zaidi, muda mfupi baada yake kuingia mamlakani.“Hii ndiyo maana zaidi ya wabunge 40 kutoka Mlima Kenya waliunga mkono hoja ya kumwondoa mamlakani,” anaeleza Bw Situma.

“Kabla ya hapo, idadi kubwa ya wabunge kutoka eneo hilo walimuasi na kutangaza kuwa Profesa Kindiki ndiye angekuwa mtetezi wao katika Serikali Kuu,” Bw Situma anaongeza.

Kwa kuonyesha kadi zake za kisiasa mapema, Gachagua aliwapa mahasidi silaha ya kumwangamiza.

Ongea machache

Nayo kanunu ya tatu yasema, Daima ongea machache ikiwezekana. Katika ulingo wa siasa Bw Gachagua alijinadi kama mtu msema kweli.

Lakini alifanya hivyo kwa kushambulia mahasidi wake kisiasa, haswa viongozi wa upinzani.

Kulingana na Bw Kabita Motua, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa, kufeli kwa Gachagua kudhibiti matamshi yake kulimkosanisha na wafuasi wake na kumtenganisha zaidi na mahasidi wake.

Usianike mafanikio

Kanuni nyingine yasema, Usianike zaidi mafanikio yako. Acha matunda ya bidii yako yaonekane yenyewe. Kila mara, Bw Gachagua alikariri mchango wake katika kufanikisha ushindi wa Rais Ruto katika eneo la Mlima Kenya.

Aminika

Kanuni ya mwisho yasema, Fanya kila uwezalo ili watu wakuamini. Dalili kuwa Gachagua alikuwa akielekea pabaya zilijitokeza Mei mwaka huu alipokosa kuhudhuria shughuli ya kitaifa ya upanzi wa miti Bomet. Rais, mawaziri na maafisa wengine wakuu serikalini walishiriki zoezi hilo.