Habari Mseto

Tume ya kusafisha Mto Nairobi yatuhumiwa kwa kuzembea kazini

Na KEVIN CHERUIYOT November 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya Madiwani wa Kaunti ya Nairobi wameibua maswali kuhusu umuhimu wa Tume ya Mito ya Nairobi ambayo imekuwa kwa miaka miwili bila kufanikisha majukumu yake.

Diwani wa Nairobi Kusini Waithera Chege ametilia shaka ushirikiano kati ya serikali ya kitaifa na ya kaunti kupitia tume hiyo katika ustawishaji wa Mto Nairobi.

Bi Waithera anaeleza kuna haja ya kuwa na mpango mwafaka kuelekeza Wakenya waelewe yanayoendelea katika shughuli ya kusafisha mto Mto Nairobi.

Kupitia taarifa, wajumbe wa kaunti wametaka serikali kuu kwa ushirikiano na Kamati ya Bunge la Kaunti kuhusu Mazingira na Maliasili kueleza iwapo kumekuwa na mfumo wa ushirikiano kati ya serikali ya kaunti na Tume ya Mito ya Nairobi.

Madiwani hao vile vile wanataka kufahamishwa majukumu mahususi ya kaunti katika ustawishaji wa mto na pesa zinazotumika katika shughuli hiyo.

“Katiba ya 2010 inatoa wito kwa serikali ya kaunti kutekeleza sera mahususi za serikali ya kitaifa kuhusu maliasili na uhifadhi wa mazingira ukiwemo utunzaji wa udongo na misitu,” alisema Bi Waithera.

 Haya yanajiri siku chache baada ya wakazi wa jiji kulalamika kuhusu hali mbaya ya Mto Nairobi baada ya Askofu Margaret Wanjiru kuteuliwa kuongoza tume hiyo.

Rais William Ruto alibuni tume hiyo Disemba 2022 ili kusaidia juhudi za kutunza mito ya Nairobi.

Katika taarifa yake, Bi Waithera alisema kuwa kamati hiyo inafaa kueleza kazi mahususi ya serikali ya kaunti katika usimamizi na utunzaji wa Mto Nairobi.

Pia, anataka wakazi wa Nairobi waelewe iwapo kuna fedha za kuwezesha Tume ya Mito ya Nairobi kutunza maliasili hiyo.

Bi Waithera aliendelea kuuliza kamati husika kufafanua mikakati ambayo Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja anakumbatia ili kuhakikisha serikali ya kaunti inashughulishwa kikamilifu katika mpango wa usimamizi na utunzaji wa Mto Nairobi.

Kulingana na Bi Waithera, kuna mkanganyiko wa majukumu na ufadhili katika mpango wa kusimamia mito na bado hakujakuwa na matokeo ya maana kwa matatizo yanayokabili Mto Nairobi.

Katika utawala uliopita wa Mike Sonko, kulikuwa na shughuli za usafi katika kingo za Mto Nairobi chini ya makundi ya vijana kupitia ushirikiano na mashirika ya kimazingira, lakini hazikufaulu kusafisha mto huo.