Makala

AMERIKA DEBENI: Wakenya wahamiaji wahofia ushindi wa Trump, nchini wakimshabikia

Na CECIL ODONGO November 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

AMERIKA, taifa lenye uchumi mkubwa duniani leo linaingia debeni, ulimwengu wote ukiwa macho kuona iwapo aliyekuwa Rais Donald Trump atarejea mamlakani au historia itaandikwa na Kamala Harris kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza nchi hiyo.

Trump aliyehudumu kama rais wa Amerika kati ya 2016-2020 analenga kurejea mamlakani kwa tikiti ya Republican huku Harris ambaye ni makamu wa rais kwa sasa akiwania kupitia chama tawala cha Democrats.

Viongozi hao wawili wamekuwa wakipishana kwa karibu kulingana na matokeo ya kura za maoni huku mshindi wa kura hiyo akitarajiwa kujulikana baadaye leo usiku au Jumatano asubuhi.

Hapa nchini, uchaguzi huo utakuwa ukifuatiliwa kwa karibu kwa kuwa karibu Wakenya 160,000 wanaishi Amerika. Tayari Wakenya ambao wanaishi Amerika wameanza kuingiwa na wasiwasi kuwa iwapo Trump atashinda kura hiyo, basi watafurushwa au kubaguliwa kutokana na sera zake

Trump, 78 amekuwa akiendeleza kampeni kali ambapo ameonekana kueneza sera dhidi ya wahamiaji na watu weusi wanaoishi au ni wazaliwa wa taifa hilo. Kwake, uwepo wa wahamiaji haramu umewapokonya raia halali wa Amerika taifa lao ndiposa kampeni zake huwa zimejaa wito wa kurejeshea Amerika ubora wake wa zamani.

Afrika kama mabara mengine yanafuatilia uchaguzi huo kwa jicho la ndani kwa kuwa kuna sera mbalimbali na maendeleo ambayo huenda yakaathirika au kuendelezwa kwa kutegemea mshindi wa uchaguzi huo.

Ingawa hivyo, Afrika ni bara ambalo Amerika huwa haijamakinikia sana kama wandani wao ambao ni mataifa ya Ulaya, washindani wao wa kiuchumi, China na pia ukanda wa Mashariki ya Kati.

Wakati wa kampeni, Trump na Harris, 60  hawajakuwa wakitaja jinsi ambavyo utawala wao utakavyoimarisha uhusiano wao na mataifa ya Bara Afrika.

Badala yake Trump na Harris wamekuwa wakizungumza kuhusu uhusiano wa Amerika na mataifa wanachama wa Muungano wa NATO hasa Uropa.

Aidha ubabe wa kibiashara kati ya China na Amerika utaathiri Afrika iwapo Trump atashinda urais. Kutokana na uongozi wake unaorejelewa kuwa wa kiimla, Trump huenda akasisitiza mataifa ya Afrika yasifanye biashara na China na ikishindikana, atataliki bara hili kabisa.

Mnamo 2019, Trump alianzisha vita vikali vya kibiashara na China katika sekta mbalimbali za kiuchumi na mataifa ya Afrika. Ilibidi marais Cyril Ramaphosa (South Africa), Paul Kagame (Rwanda) na Uhuru Kenyatta (Kenya) kukataa mpango wa kuwaondoa kwenye ushirikiano wa kibiashara na China jinsi Trump alivyotaka.

Wakati wa utawala wake, Trump alionekana kutelekeza Afrika na kila mara alikuwa akihutubu alidhalilisha bara hili kwa kutumia lugha ya maadharau. Kutokana na jinsi uongozi wake wa kwanza ulivyokuwa, ni dhahiri kuwa huenda akakosa kubadilisha fikira kuhusu Afrika na kuichukulia kama mshirika dhabiti wa kibiashara.

Kinaya ni kuwa Rais wa sasa Joe Biden ambaye hatatetei wadhifa wake kutokana na ukongwe, ameonekana kuwa na sera za kuifaa Afrika na kuondoa baadhi ya sera na vikwazo  dhalimu na kibaguiz vilivyowekwa na Trump.

Iwapo Harris atashinda uchaguzi huo, kuna uwezekano mkubwa Amerika itakuwa na ukuruba wa kuridhisha na Afrika na kuendelea na kutekeleza ufadhili wa miradi mbalimbali.

Serikali nyingi za Afrika zimekuwa zikipinga mapenzi ya jinsia moja ambayo imekuwa ikipigiwa upato na utawala wa Biden-Harris kama suala la haki za kibinadamu.

Amerika chini ya Rais Biden ilipigana vikali sana kuhakikisha kuwa inakabili mataifa mengi Afrika ambayo yalipiga marufuku mapenzi ya jinsia moja na hata kutishia kuzinyima ufadhili. Kati ya nchi hizo ni Uganda na Ghana.

Hali itakuwa tofauti iwapo Trump atarejea White House kwa sababu amewekuwa akionyesha pingamizi kuu dhidi ya mapenzi ya jinsia moja na kuyalaani.

Pia akishinda, imebashiriwa kuwa Trump ataondoa Amerika kama mwanachama wa Umoja wa Kimataifa jinsi alivyofanya mnamo 2017 baada ya kuapishwa kuchukua mamlaka.

Uchaguzi wa leo pia utakuwa na athari kwenye vita ambavyo vimekuwa vikiendelea Ukanda wa Mashariki ya Kati kati ya Israel na Palestina katika ukanda wa Gaza na vita vilivyochacha kule Lebanon.

Aidha vita ambavyo vimehudumu kwa miaka mitatu kati ya Ukraine na Urusi pia vinatarajiwa kuathirika kutokana na kura ya leo.

Rais Biden na Harris wamekuwa na uhusiano wa wastani japo mara nyingi waziwazi wamekuwa upande wa Israel kwenye vita katika ukanda wa Gaza dhidi ya kundi la Hamas. Pia Amerika chini ya Rais Biden imekuwa upande wa Ukraine kwenye makabiliano kati yake na Urusi.

Trump ni rafiki mkubwa wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu lakini amesisitiza kuwa lengo lake kuu ni kuhakikisha kuna amani Gaza na Lebanon akichukua usukani.

Hata hivyo, ni adui mkubwa wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy na akiingia mamlakani atamsaidia ‘rafikiye’ Vladmir Putin vita kati ya Ukraine na Urusi vikionekana kutoisha hivi karibuni.

Mshindi wa kura za Amerika ataamuliwa kupitia atakayeibuka kidedea katika majimbo 270 kinyume na hapa nchini ambapo mshindi huamuliwa na anayezoa kura nyingi.