Dimba

Mashabiki wahuni watishia kuharibu soka makocha wa Gor Mahia, Ingwe wakivamiwa na kupigwa baada ya mechi

Na JOHN ASHIHUNDU November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

USIMAMIZI wa Gor Mahia na AFC Leopards umetangaza kuanika wazi watu walioshambulia makocha wa timu hizo mwishoni mwa wiki.

Kocha Leonardo Neiva wa Gor Mahia na Thomas Trucha wa AFC Leopards walishambulia na watu waliodai kuwa mashabiki wa timu hizo kufuatia matokeo duni kwenye mechi za Ligi Kuu ya Kenya (FKF).

Neiva ambaye ni raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 46 alilazimika kuchana mbuga Jumamosi mjini Machakos baada ya kufukuzwa na mashabiki kufuatia sare ya 2-2 dhidi ya Murang’a Seal.

Gor walikuwa wakiongoza kwa 2-1 kabla ya Murang’a Seal kusawazisha dakika ya 94.

Awali, kocha huyo vile vile aliponea chupuchupu baada ya kikosi chake kushindwa 2-1 na Nairobi City Stars ambao walikuwa hawajashinda mechi yoyote kwenye ligi hiyo.

Naye Trucha alivamiwa na wahuni ugani Kinoru Stadium mjini Meru baada ya Leopards kuchapwa 2-0 na Ulinzi Stars, lakini usimamizi wa timu hiyo umeapa kuhakikisha waliohusika wamekabiliwa kisheria.

Akizungumza na Taifa Leo, mwenyekiti wa AFC Leopards, Dan Shikanda alisema wametambua watu 12 waliohusika kwenye njama za kumshambulia kocha wao, huku akiongeza kwamba tayari wamefikisha ripoti kwa polisi ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Kocha Neiva wa Gor Mahia amefanya mkutano na wasaidizi wake wa idara ya kiunfudi na kuweka wazi kwamba hatasimamia mechi yoyote ikiwa atafanya kazi katika mazingara kama hayo ya kuhatarisha maisha yake.

Lakini kupitia kwa mwenyekiti wa klabu hiyo Ambrose Rachier, mikakati imewekwa kuhakikisha wanaosababisha fujo wamekabiliwa kisheria.

“Nitasimamia mechi baada ya kuhakikishiwa usalama wa kutosha. Nimeuliza kuwe na maafisa wa polisi walio na silaha wakati wa mechi zetu, la si hivyo, sitaenda uwanjani, alisema kocha huyo.

Kwa upande mwingine, katibu wa Gor Mahia, Sam Ochola alidai kocha huyo anachangia katika matokeo duni yanayofuata mabingwa hao watetezi.

“Kocha alitarajiwa kusonga karibu na mashabiki kuomba msamaha lakini alipuuza mwito wa mashabiki waliomuita, sababu iliyosababisha fujo,” aliongeza Ochola.

“Nashutumu kisa hicho, lakini kocha pia alichangia kwa kiasi kikubwa. Maisha yake yatakuwa sawa iwapo ataanza kupata matokeo ya mazuri uwanjani. Natoa mwito kwa mashabiki wawe na subra wakati huu mgumu,” alisema.