Jamvi La Siasa

Viongozi waanza kumpongeza Trump anapoelekea kutawazwa mshindi

Na CHARLES WASONGA, MASHIRIKA November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa mataifa mbalimbali ya ulimwenguni wameanza kumtumia Donald Trump jumbe za kumpongeza anapoelekea kuibuka mshindi katika uchaguzi wa urais nchini Amerika uliofanyika Novemba 5, 2024.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Natanyahu na mwenzake wa Uingereza Keir Starmer wamekuwa wa kwanza kumpongeza mgombeaji huyo wa chama cha Republican baada ya kupata kura 266 za wajumbe huku makamu wa rais Kamala Harris akipata kura 219.

Kulingana na katiba ya Amerika mgombea wa urais aliyepata angalau kura 270 kati ya 538 ndiye hutawazwa mshindi.

Katika taarifa yake Netanyahu alitaja kurejea uongozini kwa Trump kama “tukio la kihistoria” huku ukiashiria “mwanzo mpya wa Amerika.

“Aidha, ushindi wa Trump utatoa nafasi na nguzu kwa ushirikiano mkubwa katika ya Israel na Amerika,” akasema katika ujumbe wake kupitia mtandao wa X.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza Starmer alisema hivi: “Nataraji kufanya kazi na Trump katika miaka ijayo.”

“Kuanzia nyanja ya uchumi, usalama, ubunifu hadi teknolojia, nijua kwamba uhusiano wa kipekee kati ya Uingereza na Amerika utaendelea kunawiri katika pande mbili tofautia za bahari ya Atlantic kwa miaka kadhaa ijayo,” Starmer akaongeza.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia alimpongeza Trump akasema yu tayari kufanya kazi naye alivyofanya katika miaka iliyopita.

“Natarajia kufanya kazi tena na Trump kwa heshima na matamanio ya kufikia mengi, na kwa ajili ya amani na ufanisi,” akaongeza.

Rais Macron pia aliongeza kuwa amefanya mazungumzo na Chansela wa Ujerumani Olaf Scholz kuhusu haja ya kupigania masilahi ya bara Uropa wanaposhirikiana na Amerika.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Hangary Viktor Orban alisema ushindi wa Trump ni “ushindi muhimu kwa ulimwengu.”

“Huu ni mwamko mpya katika historia ya kisiasa nchini Amerika,” Orban akasema katika ujumbe alioutuma kupitia mtandao wa kijamii wa X.

Bw Orban amekuwa akipigia debe kuchaguliwa tena kwa Trump katika uchaguzi wa Jumanne. Katika uchaguzi wa 2016 Waziri huyo Mkuu wa Hungary alikuwa kiongozi wa kipekee wa taifa mwanachana wa Umoja wa Ulaya (EU) kumuunga mkono Trump.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia amekuwa mwepesi wa kuchangamkia ushindi wa Trump akisema hivi:

“Natambua kujitolea kwa Trump kupalilia amani ulimwengu. Naamini kuwa ataendeleza juhudi za kuleta amani Ukraine”.

Uchaguzi wa Rais mpya sio tukio muhimu kwa Amerika pekee bali ulimwengu kwa ujumla, ikizingatiwa kuwa ni nchi yenye uwezo mkubwa duniani.

Hii ni kwa sababu Rais mpya hubadili sera ya kigeni ya nchini katika mahusiano kati yake na washirika na mahasidi wake.