Gachagua ainua mikono, aondoa kesi aliyolenga kuzima kutimuliwa ofisini
MAHAKAMA ya Rufaa imemruhusu aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua kuondoa kesi ya kutaka kusitisha kutimuliwa kwake katika Mahakama Kuu.
Kupitia kwa wakili Paul Muite, Bw Gachagua aliwaambia Majaji Patrick Kiage, Aggrey Muchelule na George Odunga kwamba suala hilo limepitwa na wakati kwa vile maagizo ya muda aliyotaka kuzuia kuapishwa kwa Prof Kithure Kindiki kuwa naibu wa rais, yaliondolewa.
Prof Kindiki aliapishwa kuwa Naibu Rais wa tatu mnamo Novemba 1, 2024 siku moja baada ya Mahakama Kuu kuondoa agizo la kumzuia kushikilia wadhifa huo.
Bw Muite alifahamisha mahakama kwamba tayari amewasilisha rufaa, akipinga mamlaka ya Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, kuteua jopo la majaji.
Mahakama Kuu iliamua kwamba mamlaka yaliyotekelezwa na Jaji Mkuu chini ya Kifungu cha 165(4) cha katiba- kuhusu uteuzi wa jopo ili kuamua masuala mazito ya kikatiba, ni ya kiutawala na Naibu Jaji Mkuu anaweza kuteua majaji kwa niaba ya Jaji Mkuu.
‘Suala hili linastahili uamuzi wake kikamilifu na tunaomba kesi iondolewe lakini mahakama itoe maagizo kuhusu rufaa hiyo,’ Bw Muite alisema.
Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor kupitia kwa wakili Prof Githu Muigai hakupinga kuondolewa kwa kesi hiyo.
Bw Gachagua aliondolewa ofisini Oktoba 17 na Rais Ruto akamteua Rais Kindiki siku iliyofuata na uteuzi wake ukaidhinishwa na Bunge la Kitaifa.
Naibu Rais aliyetimuliwa na walalamishi wengine walikimbia mahakamani na kupata agizo la kuzuia kujazwa kwa nafasi yake kusubiri uamuzi wa kesi hizo.
Wakiondoa agizo hilo Alhamisi iliyopita, majaji hao watatu walisema mfumo wa kikatiba haukunuia hali ambayo afisi ya Naibu Rais ingesalia wazi isipokuwa kipindi kifupi kinachohitajika kuijaza ikibaki wazi.
“Kwa hivyo, maslahi ya umma yanahitaji kwamba afisi ya naibu wa rais isibaki wazi,” walisema majaji.
Bw Gachagua alipinga kuondolewa kwake akishikilia kuwa mashtaka ya kuondolewa kwake hayakuthibitishwa au kuungwa mkono na ushahidi.
Alisema Bunge ilienda kinyume na katiba na kumnyima haki ya kusikilizwa kwa haki chini ya Ibara ya 25(c) na ya 50 ya katiba ilikiukwa na Seneti ilipoamua kuendelea na hoja ya kumuondoa madarakani bila kumpa fursa ya kusikilizwa. .
Naibu huyo wa rais wa zamani aliteta kuwa shughuli hiyo ilifanywa haraka kwa nia ya pekee ya kuepuka kuchunguzwa na mahakama. Bw Gachagua na washirika wake walikuwa wamewasilisha kesi 32 katika Mahakama tofauti nchini lakini hawakufaulu kusimamisha mchakato wa kumtimua katika Bunge la Kitaifa na katika seneti.
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA