Maswali mradi mpya wa nyumba nafuu ukianzishwa Voi ilhali miwili ya awali haijakamilika
MASWALI yameibuka kufuatia hatua ya serikali kuanzisha mradi mpya wa makazi mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta, huku miradi miwili ya awali ikiwa bado haijakamilika.
Mmojawapo wa miradi ya makazi ya bei nafuu wenye thamani ya Sh750 milioni, ambao ulianza miaka 12 iliyopita, bado haujakamilika kutokana na ukosefu wa fedha kutoka kwa serikali kuu.
Mradi huo, ambao ulikuwa miongoni mwa miradi mikuu ya serikali iliyopita iliyolenga kutoa makazi ya bei nafuu, sasa umewaacha wengi wakijiuliza maswali kuhusu hatima yake na athari za kuanzisha mradi mwingine mpya.
Mradi huo ulioanza mnamo 2012 chini ya Idara ya Ujenzi wa Umma na kutarajiwa kukamilika mnamo 2014, ulilenga kunufaisha zaidi ya familia 107.
Unajumuisha nyumba 36 za ghorofa zenye vyumba vitatu na nyumba 11 za kifahari zenye vyumba vya wafanyikazi. Kulingana na serikali, mradi huo ulipaswa kutekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ilikusudiwa kukamilisha nyumba 60 na awamu ya pili ilitarajiwa kukamilisha zilizosalia 47.
Ripoti kuhusu mradi huo inaonyesha kuwa ujenzi wa nyumba za ghorofa umekamilika kwa asilimia 75 na nyumba za kifahari zimekamilika kabisa.
Hata hivyo, duru za kuaminika zilidokeza Taifa Leo kuwa licha ya kuwa nyumba hizo 11 za kifahari zimekamilika, bado hazijaunganishwa na maji na hivyo kuwa vigumu kwa serikali kutafuta wamiliki.
Kazi zilizosalia katika nyumba hizo za ghorofa zinatarajiwa kugharimu takriban Sh30 milioni na zitahusisha ujenzi wa matangi ya maji machafu, njia za kutembelea kwa miguu, lango la nyumba hizo, madirisha na milango ya ndani na kuunganishwa maji na umeme.
Kampuni ya Murji Devraj na Brothers Limited, mkandarasi wa mradi huo, anaidai serikali zaidi ya Sh60 milioni kabla ya kukabidhi mradi huo kwa serikali.
Hii ni pamoja na deni la Sh30 milioni na Sh30 milioni zinazohitajika kwa ukamilishaji wa mradi. Mdokezi aliiambia Taifa Leo kuwa kampuni ya Tavevo, ambayo inahusika na kuunganisha na kusambaza maji katika eneo hilo, ilikuwa imedai Sh10 milioni ili kuunganisha maji kwenye nyumba hizo.
“Idara ya Nyumba ilisema bili hiyo iko juu sana. Walitaka kuchimba kisima, lakini maji yalipatikana kuwa hayafai,” alisema afisa mmoja wa serikali, ambaye aliomba kutotajwa jina kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari.
Mradi bado uko chini ya Idara ya Ujenzi wa Umma lakini mipango iko njiani kuuhamishia hadi kwa Idara ya Nyumba.
“Kwa miaka minne iliyopita, hali imekuwa ile ile. Hakuna kinachoendelea,” alisema. Mradi wa pili ambao haujakamilika ni ule wa Mwanyambo ambao unajumuisha nyumba 80 za vyumba viwili.
Mradi huo ambao uko chini ya Shirika la Kitaifa la Nyumba umefikia asilimia 75 na una deni la Sh30 milioni na unahitaji Sh40 milioni kukamilika.
Licha ya miradi hiyo kukwama, wakazi wameibua maswali kuhusu ujenzi wa mradi mwingine wa makazi wakati ile ya awali bado haijakamilika.
Mnamo Februari mwaka huu, serikali, kupitia Idara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji, ilianzisha ujenzi wa mradi mpya wa makazi nafuu katika eneo la Mwakingali.
Mradi huo utakaogharimu Sh1.17 bilioni unajumuisha ujenzi wa nyumba 458 zilizogawanywa katika vitengo vya kijamii, vitengo vya makazi nafuu, vitengo vya kiwango cha soko, na vitengo vya kibiashara.
Mradi huo unalenga kushughulikia mahitaji ya makazi ya jamii huku pia ukitoa huduma muhimu kwa wakazi.
Mwanaharakati wa masuala ya bajeti katika kaunti hiyo, Bi Isabella Kidede alitoa wito wa uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa fedha za umma.
Alisema serikali ilipaswa kukamilisha ile miradi mingine miwili kabla ya kuanza mradi mpya wenye thamani ya mabilioni ya fedha.
“Hakukuwa na ushirikishwaji wa umma kabla ya kuanzishwa kwa miradi hii. Tuna miradi mingine ambayo ni kipaumbele na serikali haijatekeleza na baadhi yao hata imesimama,” alisema.
Katika mahojiano ya awali, Kamishna wa Kaunti hiyo Bi Josephine Onunga alisema kuwa serikali inapania kumaliza miradi yote iliyokwama.
“Serikali ina mipango ya kukwamua miradi hiyo ili kuhakikisha kuwa pesa za mwananchi hazipotei,” alisema.