MAONI: Democrats wanafaa kujilaumu wenyewe kwa Kamala kufeli, hata ingawa Trump alitumia ujanja
KIKIHARIBIKA ni cha Fundi Mwalimu, kikifaa ni cha Bwana Su’udi. Mswahili anatoa kauli hiyo kwa mja anayeyakimbia majukumu yake na kuwalaumu watu pale mambo yanapokwenda visivyo.
Kwani kumeendaje Amerika? Mbona Kamala Harris, pamoja na uzoefu wake wa kazi, ustaarabu wa kupigiwa mfano, ufasaha wa kuzungumza, na uungwaji mkono na miamba wa chama cha Democrat ameramba sakafu katika kinyang’anyiro cha urais?
Kwani watu wenye nia njema – tulioambiwa eti watajitokeza kwa fujo kumzuia mkorofi Donald Trump wa Republican kurejea Ikulu ya White House – wamepungua nchini humo? Watawaambia watu nini? Amerika itakuwa mgeni wa nani?
Mbona mafedha yote yaliyokusanywa na chama cha Democrat, mengi tu kuliko aliyopata Trump, hayakuwasaidia kupata ushindi walioamini ni wao?
SOMA PIA: Trump ‘alivyopita nayo’ na kuduwaza ulimwengu
SOMA PIA: Jinsi Kamala Harris alivyoingia mitini na kuacha wafuasi kwa mataa alipogundua hatashinda
Mambo yameharibika katika kambi ya Democrat kwa sababu wameshindwa, na sasa karibu wanachama wote wanamlaumu Rais Joe Biden na kumwita king’ang’anizi aliyefahamu fika kwamba hakuwa na uwezo wa kutetea wadhifa wake, ila akakataa kujiengua.
Ukiwa na roho unasalitika kumwonea imani Rais huyo kwa sababu hakuna aliye na haja na nasaha yake wakati huu, licha ya kuitumikia nchi tangu ujana wake hadi akakonga na kuishiwa nguvu.
Chama chake kinamlaumu kwa kukisababishia ushinde, nao wahafidhina wa Republican wanasikia ushauri wake eti Waamerika waungane kuanzia sasa kama kelele za chura zisizomzuia ng’ombe kunywa maji. Hisia zao ni ‘amka tukae!’
Hungesikia lawama zozote
Ajabu, hungesikia lawama zozote iwapo Democrat wangeshinda uchaguzi huo. Rais Biden angesifiwa na kupongezwa kwa kuwa mzalendo wa kweli, tena kiongozi anayeona mbali kuliko kila mtu.
Hakuna anayejiuliza yeye binafsi kama mwanachama wa Democrat alichangiaje ushinde wa Kamala, wala hakuna anayetaka kukubali kwamba kampeni za chama hicho zilikosa msisimko ambao huhusishwa nacho kinapokuwa na mwaniaji mpya wa urais.
Imekuwaje kwamba maadili ya Democrat, kama vile uungwana na ujumuishaji wa watu wote katika jamii, yanashikiliwa na watu wachache ilhali maovu kama kutia hofu, chuki, ubaguzi na utengano alionadi Trump yanasisimkiwa na wengi?
Trump alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2016, Waamerika na watu wengi duniani waliamini kuwa hiyo ni hitilafu au kosa lisiloweza kurudiwa kamwe.
Visingizio vya kila aina vilitolewa, mathalan, watu wema ni wengi, hivyo kila mmoja aliamini mwenzake angejitokeza kumzuia Trump, wengi wakaishia kukaa nyumbani badala ya kwenda kupiga kura.
SOMA PIA: Uchanganuzi: Hisia za Trump kuhusu nchi za Afrika zinajulikana, hivyo haya ndiyo ya kutarajiwa…
Bila shaka haiwezekani kwamba Waamerika wamerudia kosa au hitilafu hiyo. Wanajua wanachokifanya na wameaminia kwa hakika kukifanya. Wanamhitaji Trump. Wamempima na kuona ni bora kwao kuliko Kamala.
Ukweli huu unathibitishwa na ushindi mkubwa wa Trump kwa jumla ya kura zilizopigwa kote nchini, na nyingine za wajumbe maalum kutoka kila jimbo.
Trump aliposhindana na Hillary mnamo mwaka 2016, Hillary alipata kura nyingi za jumla, ithibati ya umaarufu wake. Mara hii ni kitu gani kilichobadilika?
Ni wazi kwamba waliomchagua Trump wana sababu zao, na si lazima zipendeze kila mtu, lakini ndio wengi kwa sasa. Linalowazuga akili wanachama wa Democrat ni ukweli kwamba chama chao hakina suluhisho la masaibu yanayowakera Waamerika wengi.
Kwa tajiriba yangu ya siasa za Amerika, hasa kwa kuwa mimi ni mmoja wa vijana wengi waliobisha milango na kuwahamasisha watu wamchague Barack Obama kwa muhula wa pili mnamo mwaka 2012, nitasema Democrat walizembea mara hii!
Msisimko wa enzi za Obama haukuwepo katika kampeni ya Kamala. Mabango ya kampeni yaliyoandikwa majina yake na kauli-mbiu za kumsifia yalianza kuonekana mtaani ninakoishi wikendi iliyopita, siku mbili kabla ya uchaguzi kufanyika.
Mara yangu ya kwanza kuona jina la Kamala
Amini usiamini, mara yangu ya kwanza kuona jina la Kamala kwenye vifaa vya kampeni lilikuwa kwenye bango la Trump, bila shaka likimkashifu na kumdhalilisha.
Wanoko waliomvumisha Trump waliandika mabango ya kizushi wakionyesha madhaifu ya Kamala na kuyaangika kila mahali. Baadhi yalisema: “Trump = usalama; Kamala = uhalifu”. Jingine liliandikwa, “Trump = uchumi bora; Kamala = uvamizi wa wahamiaji”.
Karibu na ninakoishi, Mzungu fulani aliunda bendera kubwa zenye maneno hayo, akazitundika juu ya gari lake kubwa, akaliegesha karibu na sehemu iliyo na taa za barabarani hivi kwamba magari yakisimama hapo, waliomo wanasoma maandishi hayo.
Trump alipoibuka mshindi, bwana huyo aliziondoa bendera hizo, akatundika nyingine kubwa iliyoandikwa: “Mungu ameibariki Amerika!’
Maandishi ya aina hiyo yalitumika sana kubadili mawazo ya watu, tena siku nyingi tu hata kabla ya vikundi vya Kamala kutia maguu mitaani. Hata vilipowasili, havikubisha milango ya watu na kuwahimiza kumpigia kura mwaniaji wao kama tulivyofanya wakati wa Obama.
Kilichowazuia kufanya hivyo na mafedha yote waliyokuwa nayo hakijulikani, lakini hilo si muhimu tena kwa kuwa wanafuta makamasi kwa visugudi, huku baadhi ya matone ya machozi yao yakidondoka kwenye vinywaji vyao.
SOMA PIA: Trump ajitangaza mshindi wa urais, ashukuru wafuasi wake kwa kufanya makubwa
Ikiwa Jimbo la Virginia, ambalo liko takriban dakika 20 kutoka jiji la Washington D.C, yaliko makao makuu ya chama cha Democrat, linaweza kupokea vifaa vya kampeni kuchelewa hivyo, hali ilikuwaje kwenye maeneo ya mbali?
Visingizio vya kila aina vinaweza kutolewa, kwa mfano Kamala alikuwa na muda mfupi wa kufanya kampeni kwa sababu Biden alinata kama gundi, lakini ukweli ni kwamba Kamala hakuufanyia kazi wadhifa alioutaka. Alitaka cha mvunguni, mgongo ukaona ugumu kuinama.
Imedaiwa kwamba taasubi ya kiume iliwasababisha wanaume wengi Weusi na wale waliotokea Latin America kutomchagua Kamala, kisa na maana jinsia yake.
Nakumbuka Obama alipojitokeza kumfanyia Kamala kampeni aliwazomea mno wanaume Weusi kwa kujikunyata na kukaa kando wakati ambapo dada yao anawania kwa jino na ukucha kuutafuta uongozi.
Kwa maoni yangu, wanaume Weusi walishasinywa na mazoea ya chama cha Democrat kuwatafuta wakati wa kampeni pekee. Ahadi ambazo wamekuwa wakipewa na chama hicho wakati wa kampeni ni nyingi, lakini hazitekelezwi.
Nadhani baadhi yao waliamua kwamba uchaguzi hauwahusu, nao walioamua kupiga kura wakauma mdomo wa chini kukiadhibu chama cha ahadi za uongo, hivyo Kamala akafa kama kondoo wa kafara asiye na kosa.
Huwatukana kwa raha zake
Ili kuelewa kwa nini wanaume waliotokea Latin America walimchagua Trump, ambaye huwatukana kwa raha zake, badala ya Kamala, lazima uelewe utamaduni wao.
Sehemu wanakotoka, Yuda ni maarufu kuliko Yesu Kristo! Mtazamo wao ni kwamba Yuda alihitaji kuwa na akili nyingi mno ili afaulu kumsaliti Yesu. Wanapenda watu wajanja, wakora, wanaocheza shere kwa haiba kubwa.
Kwa watu hao, kwamba Trump aliwatukana tangu siku ya kwanza alipotangaza angewania urais, na matusi hayo hayajamzuia kubeba mwenge wa Republican mara tatu, ni ithibati kuwa yeye ni mtu mwerevu na mwenye nguvu sana.
Chama cha Democrat kimekuwa na changamoto ya kipekee kwa muda sasa. Kimejaa vigogo wanaoweza kumfanyia kampeni kali mwaniaji yeyote, lakini vigogo hao pia wanaweza kumgubika mwaniaji mwenyewe akafifia na kuonekana mdogo au asionekane kamwe.
Lipo swali la wazushi ambalo huibuka pale mwaniaji anapoonekana mdogo kuliko vigogo wa chama: Hivi huyu anawania yeye, au vigogo ndio wanaomtumia ili waendelee kuitawala nchi kinyemela?
Kwa taarifa yako, mpaka sasa kuna wafuasi wa Trump wanaoamini kwamba Amerika inaongozwa na Obama kwa kuwa alikuwa mkubwa wa Biden walipotawala pamoja.
SOMA PIA: MAONI: Tusidanganyane, umaarufu wa Trump umechochewa na rangi yake na itikadi kali
SOMA PIA: MAONI: Hivi demokrasia iliyokufa Tanzania, itafufuka lini?
Nadhani nia ya kumwacha Kamala ajiumbe kama mwaniaji huru ilimzuia Obama, na hata Rais Mstaafu Bill Clinton na mkewe Hillary, kujitokeza kumpigia debe.
Uungwaji mkono ambao Kamala alipata kutoka kwa mtangazaji msifika Oprah Winfrey na wasanii maarufu wa Hollywood kama vile Beyonce, Taylor Swift, Eminem na wengineo hauna thamani yoyote katika kampeni usipofuatiwa na uandikishaji wa wapigakura.
Kwanza kizazi kipya, almaarufu Gen-Z, hakina sababu ya kumshabikia Oprah. Kwao, huyo ni zilizopendwa. Hata hivyo, angeungana na kundi zima la wasanii wenzake na kuanzisha harakati za kuandikisha wapigakura, juhudi zao zingesaidia kwa kiasi fulani.
Kwa sasa, wao ni sehemu ya furushi kubwa la malofa wa Democrat wanaopaswa ama kupewa majukumu maalum kwenye chama hicho, au wapuuziliwe mbali ili kijitafutie washawishi wapya ambao vijana wanaweza kujinasibisha nao.
Yote tisa, kumi ni kwamba huu si mwisho wa dunia. Kuna matumaini. Trump atakuwa kiongozi wa mpito, kutoka kizazi kimoja hadi kingine, hivyo huenda uchaguzi utakaofanyika mwaka 2028 utavutia wawaniaji usiowahi kuwasikia. Ni hulka ya Amerika kujigeuza upya na kupata umaridadi mpya kwa kujibambua ngozi kama nyoka.