DimbaMakala

Hivi huyu Amorim ndio atakuwa Mourinho mpya pale Man Utd?

Na MASHIRIKA November 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MANCHESTER, UINGEREZA

HUKU akiwa tayari amepachikwa jina la ‘The New Special One’ kwa maana ya Jose Mourinho mpya, kocha wa Manchester United, Ruben Amorim amesema yuko tayari kabisa kuanza kazi, huku akisisitiza kwamba atatekeleza wajibu huo akishirikiana na wasaidizi wake waliofuatana naye kutoka Sporting Lisbon.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 39 amekataa kabisa kujumuisha Ruud van Nistelrooy kwenye idara yake ya kiufundi, hata baada ya Mholanzi huyo kuwezesha United kutoshindwa katika mechi nne baada ya kuchukuwa usukani kama kaimu kocha wa vigogo hao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Nistelrooy ambaye ni mshambuliaji wao wa zamani, ameondoka Old Trafford baada ya kuandikisha ushindi mara tatu na sare moja katika mechi nne, ukiwemo ushindi mkubwa wa 3-0 dhidi ya Leicester City katika mechi ya EPL siku ya Jumapili.

Hii si mara ya kwanza kwa Amorim kuwa Old Tafford, kwani aliwahi kumsaidia Jose Mourinho kunoa Manchester United hapo awali.

Amorim ana siku 11 pekee kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza – United watakapokuwa ugenini kucheza na Ipswich Town, huku akitarajiwa kutumia mfumo wake wa 3-4-3 aliotumia akiwa na Sporting Lisbon.

Kocha huyo amewasili Old Trafford kuongoza kikosi ambacho hakifurahishi mashabiki kutokana na matokeo duni tangu msimu uanze- huku baadhi ya wachezaji wakikabiliwa na majeraha.

Kocha huyo anayepanga kushawishi mastaa wawili kutoka Sporting wajiunge na United anatarajiwa kuwa na kikosi imara iwapo nyota wanaokabiliwa na majeraha watapata nafuu kabla ya mechi ijayo.

Kwa mujibu wa tetesi za wataalamu wa masuala ya soka nchini hapa, kipa Andre Onana na Altay Bayindir ni miongoni mwa watakaotegemewa chini ya kocha huyo mpya, sawa na kinda Leny Yoro ambaye amerejea baada ya kuvunjika mfupa wakati wa mechi za maandalizi kabla ya ligi kuanza.

Kuna wachezaji akiwemo beki wa katikati Matthijs de Ligt ambao hawajaonyesha makali jinsi ilivyotarajiwa, lakini chini ya Amorim, huenda wakabadilika na kurejea katika viwangao vyao bora.

Lisandro Martinez, raia wa Argentine hakuvuma sana wakati wa kocha Erik ten Hag, lakini anatarajiwa kuhifadhi nafasi yake kikosini, sawa na Diogo Dalot aliyefanya makosa katika eneo la hatari mara kwa mara chini ya Ten Hag. Vile vile, huenda Kobbie Mainoo akapendelewa badala ya Casemiro kama kiungo mkabaji.

Nyota wa Ureno Bruno Fernandes anatarajiwa kubakia kama nahodha, hata iwapo kiwango chake kitashuka.

Noussair Mazraui na Luke Shaw watapata nafasi kikosini iwapo watapata nafuu kutokana na majeraha, wakati Marcus Rashford na Rasmus Hojlund wakitarajiwa kujitahidi ili waendelee kuongoza safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikibabaisha.

Amorim vile vile atamtegemea Alejandro Garnacho ambaye amekuwa winga moto msimu huu.