Makala

Ripoti yafichua hali bado ngumu madeni yakifyonza mabilioni ya pesa za umma

Na BENSON MATHEKA November 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

PESA ambazo Kenya inatumia kulipa deni la nje ziliongezeka karibu maradufu katika mwaka wa fedha uliokamilia Juni 2024 na  kufikia Sh756 bilioni huku serikali ikizidisha juhudi za kupunguza utashi wake wa mikopo ya ndani ambayo imefinya sekta ya kibinafsi.

Kuongezeka kwa pesa za kulipa deni  kumechangiwa zaidi na kukomaa  kwa mkopo wa Eurobond wa Sh260 bilioni ambao uliweka nchi katika hali ngumu ya kifedha katika nusu ya kwanza ya mwaka wa kifedha wa 2023-2024.

Ripoti mpya ya Hazina ya Kitaifa kuhusu deni la umma inasema kwamba pesa pesa za kulipa  deni la nje la nchi zilipanda kutoka Sh402.4 bilioni hadi Sh756 bilioni, ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliotangulia.

Katika mwaka wa fedha wa 2022-23, pesa za kulipa deni la nje ziliongezeka kwa Sh96 bilioni. Ripoti hiyo pia inaonyesha serikali ilitumia Sh807 bilioni kulipia deni la ndani huku jumla ya deni la umma sasa likiwa Sh10.6 trilioni.

Deni la ndani la umma kwa asilimia ya deni lote sasa ni asilimia 51 likiongezeka kutoka asilimia 47 mwaka wa fedha wa 2022-23 huku deni la nje likipungua hadi asilimia 49  kutoka asilimia 53 mwaka 2022-23.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa mbele ya Bunge la Kitaifa inasema kwamba hadi kufikia mwisho wa Juni 2024, deni la ndani lilikuwa Sh5.4 trilioni. Hili ni ongezeko la Sh578 bilioni,  ambalo ni asilimia 12 zaidi ya deni la ndani la Sh4.8 trilioni kufikia mwisho wa Juni 2023.

Katibu  wa Hazina ya Kitaifa Chris Kiptoo alisemawakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo wiki jana kuwa Sh1 trilioni zimetengwa kulipa deni la umma katika mwaka huu wa kifedha. Kati ya fedha hizo, Sh750 bilioni zitalipa deni la ndani.

Dkt Kiptoo alieleza  imani kuwa juhudi za Benki Kuu ya Kenya za kurekebisha soko la fedha za kigeni na kudhibiti viwango vya riba zitakuwa na jukumu muhimu katika kuhakikisha serikali haitumii pesa nyingi kulipia deni la umma.