Ruto alivyojitetea mbele ya Uhuru kuhusu maendeleo
RAIS William Ruto mnamo Jumamosi, Novemba 16, 2024 alijitetea vikali mbele ya aliyekuwa bosi wake, Uhuru Kenyatta, jinsi alivyoendeleza kazi aliyomwachia.
Bw Kenyatta, ambaye kwa sasa ni rais mstaafu, alihudumu kama Rais wa Nne wa Jamhuri ya Kenya mihula miwili (2013 – 2022), Dkt Ruto akiwa naibu wake.
Akihutubu katika hafla ya kutawazwa kwa Askofu Peter Kimani Ndung’u wa Kanisa la Katoliki, Dayosisi ya Embu, Rais Ruto alimweleza mtangulizi wake kwamba majukumu aliyotwaa anazidi kuyasukuma mbele.
Bw Kenyatta, alikuwa miongoni mwa wageni na viongozi mashuhuri waliohudhuria utawazo wa Askofu Kimani, kwenye hotuba yake akimtaja Kasisi huyo kama rafiki wake wa karibu.
Akionekana kujikakamua, Ruto alisema anapambana kutekeleza majukumu aliyoachiwa na bosi wake wa kitambo.
“Kiongozi wetu aliyestaafu, Rais Uhuru Kenyatta, kazi uliyoniachia mimi nang’ang’ana nayo mbaya sana, napambana nayo…” Rais Ruto alisema, umma ukishangilia.
Kiongozi wa nchini alitumia jukwaa hilo kuainisha sera zake, na miradi aliyofanya.
Hata ingawa umma uliskika ukinung’unika, alitaja mpango tata wa afya bora kwa wote wa SHIF unaotekelezwa na mamlaka ya SHA, na vilevile mradi wa nyumba za bei nafuu, kama miradi aliyofanikisha.
Kwa upande wake Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta, aliyehutubu kabla ya Dkt Ruto, alionekana kukwepa masuala ya siasa, akisema lake “ni kujitazamia runinga na kuskiza redio”.
Hafla ya kutawazwa kwa Askofu Kimani ilifanyika katika Chuo Kikuu cha Embu, na alipoingia na kuondoka, Bw Kenyatta alishangiliwa na kufurahiwa na umma.
Naibu Rais aliyebanduliwa, Rigathi Gachagua, na mrithi wake, Prof Kithure Kindiki pia walikuwepo.
Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Kenyatta alikuwa anaunga mkono kinara wa Azimio, Raila Odinga, hatua ambayo haikuonekana kumuendea vizuri Dkt Ruto aliyeibuka kidedea kupitia tikiti ya muungano wa Kenya Kwanza.
Bw Odinga, hata hivyo, kwa sasa anashirikiana sako kwa bako na Rais Ruto, kiongozi wa nchi akijitolea kwa hali na mali kufanyia kampeni Waziri Mkuu huyo wa zamani kupata wadhifa wa uenyekiti AUC.