Atakayempuuza Jumwa ‘Simba Jike’ wa Kilifi 2027 atajua hajui!
NI takriban miezi mitano tangu Rais William Ruto kufutilia mbali baraza lake la mawaziri wakati wa maandamano ya vijana wa Gen-Z waliokuwa wanapinga Sheria ya Fedha ya 2024.
Mmoja wa waziri aliyetimuliwa alikuwa Bi Aisha Jumwa aliyekuwa akiongoza wizara ya Jinsia na mwanamke wa pekee pwani kuwa katika wadhifa huo.
Swali vinywani mwa wengi ni iwapo Bi Jumwa atapewa tena kazi katika serikali Kenya Kwanza.
Hii ni ikizingatiwa kuwa alikuwa mwanasiasa mtajika katika kampeni za Kenya Kwanza.
Wakati wa ziara yake pwani,Rais Ruto alisema kuwa hatamwacha Bi Jumwa kwani atamjumuisha katika serikali yake.
Kulingana na wachanganuzi wa siasa, Bi Jumwa ni mwanasiasa ambaye serikali ya Kenya Kwanza au chama cha United Democratic Alliance (UDA) hakifai kumtupa kwani ana wafuasi kadhaa ambao wanaweza kusaidia chama hicho.
Mchaganuzi wa siasa Bw Abdulrahman Abdalla anasema kuwa Bi Jumwa ni kiongozi mashuhuri katika ukanda wa pwani ambaye siasa zake zinaweza kusaidia muungano wa Kenya Kwanza.
“Kwa kusema kweli Bi Jumwa anao ushawishi mkubwa wa kisiasa sio tu katika kaunti ya Kilifi atokako bali ukanda wa pwani kwa jumla. Ni mwanasiasa muhimu sana kwa Kenya Kwanza iwapo kinadhamiria kupata uungwa mkono pwani,” akasema Bw Abdalla. Anaongeza kuwa Bi Jumwa pia anayo nafasi ya kuwania nafasi ya uongozi katika chama cha UDA.
Aisha Jumwa ana ufuasi mkubwa ambao haufai kupuuzwa
“Si rahisi lakini Bi Jumwa ni mwanasiasa ambaye anaweza kuwania nafasi katika chama cha UDA na kumweka katika nafasi ya uongozi wa chama,”alisema Bw Abdalla.
Ikumbukwe kuwa Bi Jumwa aliwania ugavana kwa tikiti ya UDA katika uchaguzi uliopita ingawa alishindwa na gavana wa sasa wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro.
Mchaganuzi wa siasa za ukanda wa pwani ambaye pia ni mtaalam wa mawasiliano Bw Kauli Mwatela anasema kuwa Bi Jumwa si mwanasiasa wa kupuuzwa katika ukanda wa Pwani.
“Iwe ni chama cha UDA au kingine, Bi Jumwa ana ushawishi mkubwa na wafuasi wengi katika ukanda wa pwani, kwa hivyo anayempuuza atajuta wakati wa uchaguzi ujao,”alisema Bw Mwatela.
Anaongeza kuwa kwa sasa Bi Jumwa licha ya kutokuwa na wadhifa wowote katika serikali, ndiye mwanamke mwanasiasa mtajika katika ukanda wa pwani.
Kwa wakazi wa pwani na wafuasi wa Bi Jumwa, wanaangalia iwapo atapewa nafasi yoyote ya uongozi katika serikali ya Kenya Kwanza.