Hawa Liverpool wamekuja kivingine msimu huu!
KINYUME na ilivyotarajiwa na wengi, kocha Arne Slot hajatatizika kabisa kujaza pengo lililoachwa na Jurgen Klopp kambini mwa Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita wa 2023-24.
Badala yake, Mholanzi huyo anazidi kuwapa mashabiki kitu kipya cha kufuatilia ugani Anfield; na tayari ameongoza Reds kuanza kampeni za muhula huu kwa matao ya juu huku akivunja rekodi ya miaka 20 katika mchakato huo.
Baada ya kupepeta Bayer Leverkusen 4-0 katika pambano la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 5, 2024, Liverpool sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la kipute hicho kwa alama 12 kutokana na mechi nne.
Isitoshe, wanadhibiti kilele cha jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa pointi 28 baada ya kushinda mechi tisa, kupiga sare mara moja na kupoteza mchuano mmoja kati ya 11 iliyopita. Aidha, wametikisa nyavu za wapinzani wao ligini mara 21 huku magoli sita ambayo wamefungwa yakiwafanya kuwa kikosi kilichopachikwa mabao machache zaidi kufikia sasa katika EPL msimu huu wa 2024-25.
Liverpool, ambao wamefungwa bao moja pekee katika UEFA muhula huu, walianza kivumbi hicho kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya AC Milan ugenini kabla ya kufinya Bologna 2-0 nyumbani na kutandika RB Leipzig 1-0 nchini Ujerumani. Kikosi hicho kimepoteza mechi moja kati ya 17 za kwanza chini ya Slot aliyetokea Feyenoord ya Uholanzi.
Kwa hakika, Liverpool wameshinda michuano 15 kati ya 17 iliyopita na kumfanya Slot, 46, kuwa mkufunzi anayejivunia mafanikio makubwa zaidi katika historia baada ya mechi 16 za kwanza akidhibiti mikoba ya klabu ya EPL.
Slot sasa amemdengua Jose Mourinho kwenye orodha hiyo ya makocha, baada ya ‘Special One’ kushinda mechi 13 kati ya 16 za kwanza alipowasili Chelsea kwa mara ya kwanza mnamo 2004. Carlo Ancelotti aliifikia rekodi hiyo ya Mourinho katika muhula wake wa kwanza ugani Stamford Bridge mnamo 2009.
Slot amewapiku wakufunzi wengine kadhaa waliowahi kufikia ufanisi huo, akiboresha rekodi za makocha watatu wa zamani wa Chelsea – Avram Grant, Antonio Conte na Maurizio Sarri – ambao walishinda mechi 12 kila mmoja kutokana na 16 za kwanza. Unai Emery naye alishinda michuano 12 kati ya 16 ya kwanza aliyosimamia kambini mwa Arsenal alipomrithi kigogo Arsene Wenger mnamo Mei 2018.
Pointi tano pekee ambazo Liverpool wamedondosha katika EPL msimu huu ni dhidi ya Nottingham Forest waliowakomoa 1-0 ugani Anfield mnamo Septemba 14, wiki sita kabla ya kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Arsenal uwanjani Emirates.
Ingawa hivyo, huenda uthabiti wa Liverpool ukawekwa kwenye mizani kamili katika mechi tatu kati ya nne zijazo dhidi ya Southampton, Real Madrid, Manchester City na Newcastle United kwa usanjari huo.
Hata hivyo, Slot haonekani kutikiswa kabisa na ugumu wa kibarua kinachowasubiri vijana wake huku akisisitiza kuwa Liverpool wanalenga kupigania mataji ya mashindano yote msimu huu.
Akizungumza baada ya ushindi wao dhidi ya Leverkusen, alisema: “Katika nafasi yetu kwa sasa, bila shaka kuna shinikizo kubwa japo ni sisi wenyewe tumetaka kuwa mahali hapo tulipo. Hilo ni jambo linalotuchochea kujituma sana. Ukivalia jezi za Liverpool, unajua ni mchezaji yupi wa akiba atakunyima namba kabisa akianza kuletwa uwanjani. Kocha naye ana presha kali kwa sababu anajua mrithi wake yuko tayari wakati wowote. Itahitaji mabosi kunyanyua simu tu…”
Liverpool ni mabingwa mara 19 wa EPL na wafalme mara sita wa UEFA (1977, 1978, 1981, 1984, 2005, 2019). Walinyanyua taji la EPL mara ya mwisho mnamo 2019-20 kwa pointi 99 baada ya kusubiri kwa miaka 30. Waliambulia nafasi ya tatu msimu uliopita baada ya kujizolea alama 82, saba nyuma ya Arsenal na tisa zaidi nyuma ya Man-City waliotwaa kombe hilo kwa mara ya nne mfululizo.
Makocha wapya wa EPL walioshinda mechi nyingi zaidi baada ya 16 za kwanza katika mashindano yote:
- Arne Slot: 14 (Liverpool, 2024)
- Jose Mourinho: 13 (Chelsea, 2004)
- Carlo Ancelotti: 13 (Chelsea, 2009)
- Avram Grant: 12 (Chelsea, 2007)
- Antonio Conte: 12 (Chelsea, 2016)
- Unai Emery: 12 (Arsenal, 2018)
- Maurizio Sarri: 12 (Chelsea, 2018)
Mechi nne zijazo za Liverpool:
- Novemba 24:Southampton vs Liverpool (A)
- Novemba 27:Liverpool vs Real Madrid (H)
- Desemba 1:Liverpool vs Man-City (H)
- Desemba 4:Newcastle vs Liverpool (A)
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO