Habari za Kitaifa

Maoni: Uhuru, Gachagua waungane kumzima Ruto Mlima Kenya

Na CECIL ODONGO November 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta anastahili kuungana na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhakikisha kuwa Mlima Kenya inatoa mwaniaji wa urais 2027 na kumpeleka Rais William Ruto nyumbani.

Kwenye uchaguzi wa 2022, Mlima Kenya ulionyesha uaminifu mkubwa kwa Rais Ruto na kumpigia kura licha ya kuwa kiongozi wao mkuu wakati huo Bw Kenyatta alikuwa akimuunga mkono Kinara wa Upinzani Raila Odinga.

Wapigakura wa mlimani walimpa Rais Ruto asilimia 87 za kura na kwenye idadi ya kura milioni 7.1 ambazo Rais alijizolea, karibu milioni nne zilitoka kwenye kapu lao.

Ni wakati ambapo viongozi na wakazi wa Mlima Kenya wanastahili kuthamini idadi ya kura walizonazo na kuzitumia aidha kuingia serikalini au kuingia katika miungano baada ya uchaguzi mkuu.

Kati ya sababu ambazo zilimsaidia Bw Kenyatta kuingia mamlakani mnamo 2013 ni idadi ya kura za Mlima Kenya na Bonde la Ufa, ambapo jamii kutoka maeneo hayo mawili zilithamini na kututumia idadi yao vyema.

Wakati huo, Rais Kibaki ambaye pia alikuwa akitokea mlimani alikuwa akikamilisha muhula wake na wengi walitarajia kuwa ingekuwa vigumu sana kwa rais mpya kutoka ukanda huo.

Kwa kipindi kimoja, Bw Kenyatta alitupilia mbali azma yake na kukubali kumuunga mkono Musalia Mudavadi japo wajumbe wa TNA baadaye walimkabili, wakamkataza na kusema liwe na liwalo lazima asimame.

Kilichofanya Bw Kenyatta awanie urais wakati huo badala ya kuwa naibu wa Ruto ni kwa sababu takwimu zilionyesha kuwa alikuwa na kura nyingi kutoka ngome yake ya kisiasa kuliko Ruto.

Ushirikiano wa wawili hao ulihakikisha kuwa wanapata ushindi kwa kuzoa kura kutoka Bonde la Ufa na Mlima Kenya na kumbwaga waziri mkuu wa wakati huo Bw Raila Odinga.

Kutokana na tukio lililoshuhudiwa Embu wikendi, ambapo wananchi waliwachangamkia Uhuru na Gachagua, wakati umetimia ambapo wanasisa hao wawili wanastahili kuhakikisha kuwa jamii hiyo inatumia idadi yake ya kura kwa manufaa yao kisiasa.

Jamii haiwezi kuwa na zaidi ya kura milioni nne kisha inahangaishwa na hata kigogo wao wa kisiasa kuondolewa kimadharau jinsi ambavyo Bw Gachagua alifanyiwa mwezi uliopita, Oktoba 2024.

Ukweli ni kuwa kwa sasa Mlima Kenya upo upinzani kwa sababu ya makosa waliyofanya 2022 ambapo waliingia kwenye ushirikiano na Rais Ruto bila chama chochote cha kisiasa.

Mabw Kenyatta na Gachagua wanastahili kusaka chama kingine cha kisiasa kwa sababu ni dhahiri kuwa kwa sasa wakazi wa Mlima Kenya hawako UDA.

Kuwa na chama cha kisiasa kutahakikisha kuwa eneo hilo linapata wabunge wao ambao hawatashawishiwa na watu wa vyama vingine ikifika wakati wa kumpiga vita nyapara wao wa kisiasa.

Afadhali Mlima Kenya iwe na mwaniaji wa urais ambaye hata akianguka debeni anaweza kutumia idadi ya kura na wabunge wake kuingia kwenye muungano na mshindi.

Hali hii itakuwa afadhali kuliko kumuunga mwaniaji kutoka nje ya eneo hilo kisha akishinda, tofauti za kisiasa zinazuka na anaishia kwenye kijibaridi cha kisiasa kama Bw Gachagua.