Wagonjwa wazidi kuhangaika chini ya Bima ya SHIF licha ya hakikisho la serikali
BIMA mpya ya Afya ya Jamii (SHIF) inaendelea kuwahangaisha wagonjwa wanaotafuta huduma katika hospitali mbalimbali.
Bi Racheal Elegosa aliyepata majeraha mabaya kichwani baada ya kuanguka na kutibiwa, amezuiwa kwa zaidi ya siku tano katika hospitalini ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) Kaunti ya Kisumu.
Dada yake Mary Kwangwa amekuwa akikimbizana na mfumo wa mawasiliano ya SHIF utume ujumbe kutoka Mbale, Kaunti ya Vihiga ili akamilishe salio la ada ya hospitali ya Sh64,307.
Bi Elegosa amekuwa hospitalini tangu Novemba 10, 2024 akitibiwa kuondoa mgando wa damu kwenye ubongo.
“Tulipopeleka mgonjwa katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Vihiga ambapo tulilipia huduma kupitia SHA na tukaelekezwa kuenda JOOTRH. Lakini sasa JOOTRH inahitaji ushahidi kuonyesha tulilipa, ama tulipe salio kwa pesa taslimu na hali hatuna uwezo wa kulipa,” akaambia Taifa Leo.
Simulizi ya Bi Mary ni sawa na ya Bi Jane Otieno ambaye alimpeleka mgonjwa wa saratani katika hospitali hiyo ya kanda mnamo Novemba 14.
Mgonjwa huyo ambaye amesajiliwa chini ya bima ya SHIF alipuuzwa kwa sababu mfumo wa hospitali hiyo haukuonyesha amesajiliwa katika bima hiyo.
“Awali walituambia dawa hazikuwa na wakatuomba tuje leo (Jumatatu). Sasa wanasema SHA haijaweka maelezo yetu ya usajili katika SHIF. Tunafaa kufanya nini sasa?” akateta.
Visa hivi vinaashiria matatizo makubwa yanayowakumba wakazi wengi ambao wanategemea mfumo mpya wa bima nchini.
Meneja wa Jiji la Kisumu Abala Wanga hivi maajuzi alikemea serikali ya kitaifa kwa kutotatua changamoto za SHIF upesi.
“Mpito (kutoka NHIF hadi SHIF) umekuwa janga. Unatarajia kuendesha hospitali vipi wakati malipo ya SHA yanachelewa kwa miezi kadhaa?” Bw Wanga aliteta wakati wa uzinduzi wa Kitengo cha kushughulikia Dharura ya Ajali katika Hospitali ya Avenue juma lililopita.
Waziri wa Afya Deborah Barasa ameteta uzinduzi wa SHA akisema umepiga hatua.
“JOOTRH imepokea malimbikizo ya madeni ya NHIF na kufikia mwisho wa Novemba, watapata malipo ya kwanza ya SHA,” alisema Dkt Barasa alipokuwa akikagua hospitali hiyo Jumatatu.
Vile vile, alidokeza kuwa wagonjwa wanane kati ya kumi wamekuwa wakinufaika kwa bima ya SHIF katika kitengo cha tiba ya figo.