Shangazi Akujibu

Mume haniamini kabisa anadhani nina mpango wa kando

November 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Hujambo shangazi? Kuna tatizo limeingia katika ndoa yangu. Mume wangu haniamini. Mara nyingi nisipokuwa nyumbani hufikiria nina mwanamume mwingine. Sijawahi kwenda nje ya ndoa na tabia yake hiyo inaniudhi sana. Nifanyeje?

Mume wako anasumbuliwa na wivu. Hawezi kukufungia nyumbani ili usionekane na wanaume wengine. Endelea kumhakikishia uaminifu wako kwake. Hatimaye atathibitisha huna mambo mengine nje ya ndoa kisha atatulia.

Nimempenda mubaba

Nina umri wa miaka 18 na ninasoma katika shule ya upili. Nimependana na mwanaume wa miaka 35 na ameahidi kunioa. Je, ni makosa?

Hayo ni makosa makubwa. Wewe bado ni mdogo sana, huna uwezo wa kuelewa mapenzi. Utaharibu maisha yako. Mwambie mwanaume huyo asubiri umalize masomo.

Msupa ninayempenda anadai dume linalozuru kwake ni rafiki tu, ila siamini!

Za kwako shangazi. Nampenda mwanamke jirani yangu na nimeona dalili kuwa yeye pia ananitaka. Lakini kuna mwanamume ambaye nimempata kwake mara kadhaa. Aliniambia ni rafiki tu lakini siamini. Nishauri.

Ni jambo la kawaida kwa wanaume kadhaa kumtaka mwanamke mmoja. Mwanamke huyo ndiye ataamua ni nani anayemfaa kati yako na huyo mwanamume mwingine. Kama kweli unampenda, usife moyo.

Anataka kurudi ila mimi sina nafasi yake tena moyoni

Nilitofautiana na mpenzi wangu kuhusu mambo fulani na tukaachana. Tangu hapo amekuwa akinipigia simu akitaka turudiane na mimi sitaki. Naomba ushauri wako.

Mwanamume huyo ameonyesha nia ya kufufua uhusiano wenu. Kama umeamua huwezi kurudiana naye, sidhani unahitaji ushauri wangu. Mwambie wazi kwamba humtaki ili aondoe mawazo yake kwako.