NAKURU: Hofu utengenezaji wa maji bandia kuongezeka
NA RICHARD MAOSI
Wakazi wa kaunti ya Nakuru wamekuwa wakielezea hofu yao baada ya washukiwa kadhaa kunaswa wakitengeneza maji bandia katika makazi ya kibinafsi bila stakabadhi rasmi kutoka kwa idara ya afya kwa umma .
Muda wa wiki moja iliyopita ufichuzi wa Taifa Leo Dijitali ulibainisha ongezeko la idadi ya wachuuzi wa maji bandia ya chupa, mjini Nakuru yanayouzwa kwa bei nafuu.
Operesheni inayoendelea kufanywa na walinda usalama kuanzia wiki iliyopita, imezaa matunda ambapo maji bandia yalipatikana na washukiwa wanne na kukamatwa.
Aidha nembo ya ubora wa bidhaa (KEBS) iliyotumika katika sehemu za chupa ilikuwa ni bandia. .
Naibu kamishna wa Nakuru West Elmi Shafi anasema polisi walifanya msako katika makao ya wahalifu baada ya kupata taarifa kutoka kwa umma.
Anasema utengenezaji maji ulikuwa ukifanyika katika makazi ya mtu binafsi mtaani Kibera eneo la Rhonda viungani mwa Nakuru.
Wafanyikazi watatu waliopatikana katika eneo la tukio pamoja na mshukiwa mwingine wa kike ambaye ndiye mmiliki halisi hawakuepuka mkono wa sheria.
alikamatwa mjini Nakuru katika duka lake la kijumla analotumia kusambaza maji ya ‘Cool drop spring’ kwa wachuuzi mjini.
“Bila kupoteza muda tulikabiliana na wahusika kwa kuhatarisha maisha ya raia.Washukiwa watatu pamoja na bosi wao walifikishwa katika kituo cha polisi cha Central wakisubiri kukabiliana na mkono mrefu wa sheria,”Shafi alisema.
Polisi walifanikiwa kuharibu mtambo wa kutengeneza maji ambao kulingana na wizara ya afya kwa umma, ni haramu kisheria.
“Tulizungumza na idara husika na wakadhibitisha kuwa masine yenyewe haikufaa kutumika na kwa sababu haizingatii kiwango cha usafi unaohitajika,”alisema.
Chifu wa eneo la Rhonda Peter Kirui alisisitiza amekuwa akifuatilia kwa karibu mmiliki wa ploti ambapo maji yalikuwa yakiundwa .
Lakini alitoroka alipopata fununu polisi wanamsaka kwa kuruhusu makazi yake kuwa karakana ya bidhaa haramu.
“Bado tunamtafuta mwenye ploti aliyewaficha wahalifu,pia alikubali maji kutekwa kutoka kisimani na kupakiwa ndani ya chupa.Tunawaomba wakazi wakome kutumia maji haya,”alisema.
Tulipozuru eneo la tukio tulibaini maji huvutwa kutoka kisimani kwa mtambo unaotumia umeme kisha yakahifadhiwa ndani ya tanki lilifukiwa ardhini.
Maji hayo huelekezwa katika tanki nyingine ndani ya nyumba ambapo husafishwa na kuunganishwa kwa mfereji .
Baadhi ya wakazi tuliozungumza nao walitetea waendeshaji mradi huo wakisema NAWASCCO walikuwa wameshindwa kuwapatia maji.
“Serikali ya kaunti imeshindwa kutupatia maji kwa wakati ufaao,tunashindwa ni kwa nini Bi Maria Muthoni amekamatwa,”Joseph Kuria mkaazi alisema.
Kulingana na afisa mkuu wa Department of Public Health Samwel Kingori anasema ni wajibu wa serikali kuhakikisha raia uhalali wa bidhaa.
Pia anawasuta rakazi kwa kumtetea mhalifu anayehatarisha maisha yao,akisema wawatumie viongozi wao kuwakilisha malalamishi yao.
“Wakazi wa Rhonda waliwateua viongozi wana kila sababu ya kuitisha haki zao za kimsingi kama vile maji na huduma nyinginezo,”alisema.