Mwachilieni Besigye, viongozi wa upinzani Afrika washinikiza Uganda na Kenya
VIONGOZI wa upinzani Afrika wameshinikiza kuachiliwa huru kwa kiongozi wa upinzani Uganda Kizza Besigye.
Mwanasiasa huyu anadaiwa kutekwa nyara jijini Nairobi Jumamosi iliyopita.
Viongozi wa upinzani barani wamelaani mienendo ya serikali za mataifa ya Afrika wanazosema zinaendeleza vitendo vinavyokiuka sheria.
Kwenye taarifa ya Jumatano, Novemba 20, 2024 wanachama wa muungano wa viongozi hao (PAOLSN), tawi la Afrika Mashariki, wanadai Dkt Besigye alitekwa nyara na maafisa wa usalama wa Kenya wakishirikiana na wenzao wa Uganda.
“Tukio hilo linaudhi na kuogofya zaidi. Tunashuku kuwa Dkt Besigye huenda alitekwa nyara baada ya kufikishwa katika jengo la Riverside Apartment. Na waliohusika ni maafisa wa usalama wa Uganda wakisaidiana na maafisa wa usalama wa Kenya,” muungano huo, Pan African Opposition Leaders Solidarity Network, ukasema kwenye taarifa iliyotiwa saini na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua.
“Tunataka vyombo vya usalama nchini Kenya, haswa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kufichua aliko Dkt Besigye. Utekaji nyara unaoendeshwa na maafisa wa usalama ni kinyume cha sheria ya ushirikiano kati ya Kenya na Uganda. Huu ni ukiukaji wa sheria za nchi husika na sheria za kimataifa,” taarifa hiyo ikaongeza.
Hata hivyo, msemaji wa polisi nchini Kenya Dkt Resila Onyango amekana madai kuwa Dkt Besigye, ambaye ni kiongozi wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) alitekwa nyara nchini Kenya.
“Hatuna habari zozote kuwa mwanasiasa wa Uganda Kizza Besigye alitekwa nyara. Kutoweka kwake hakumaanishi kuwa amatekwa nyara. Hata hivyo, uchunguzi unaendelea kuhusu kisa hicho,” akasema.
Dkt Besigye ambaye aliwasili nchini Kenya kwa ajili ya kuhudhuria uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na Bi Karua, alitoweka Jumamosi jioni katika jengo la 108 Riverside Apartment eneo la Westlands jijini Nairobi ambako ilisemekana alienda kukutana na ‘watu fulani.’
Alikuwa amekodisha chumba cha kulala katika mkahawa wa Waridi Paradise Hotel and Suites ulioko katika mtaa wa Hurlingham, Nairobi.
Kiongozi huyo wa upinzani Uganda alitarajiwa kuwa miongoni mwa wahutubu Jumapili Novemba 17, 2024 katika halfa ya uzinduzi wa kitabu cha “Against the Tide” kinachoelezea pandashuka za kisiasa za Bi Karua.
Mkewe Besigye Winnie Byanyima, ameitaka serikali ya Uganda imwachilie huru mumewe anayeshuku amezuiliwa katika gereza moja la kijeshi jijini Kampala nchini humo.
“Naiomba serikali ya Uganda imwachilie huru mume wangu Dkt Kizza Besigye mara moja. Alitekwa nyara Jumamosi jijini Nairobi alikoenda kuhudhuria uzinduzi wa kitabu cha Mheshimiwa Martha Karua,” Bi Byanyima akaandika Jumatano Novemba 20, 2024 katika akaunti yake ya mtandao wa X.
Wakati huo huo, serikali ya Uganda imevunja kimya chake kuhusu suala hilo ikishikilia kuwa haina habari kuhusu kutoweka kwa Dkt Besigye.
Katika mahojiano na gazeti la “Daily Monitor” Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Mwongozo wa Kitaifa, Chris Baryomunsi, alikana kuwa na habari kuhusu kisa hicho na kusema serikali itafanya uchunguzi kubaini ukweli.