• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Mudavadi ataka jopo la maridhiano kuitisha mkutano Bomas

Mudavadi ataka jopo la maridhiano kuitisha mkutano Bomas

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi ameitaka Kamati ya Maridhiano (BBI) kuitisha kongamano la kitaifa kujadili masuala yaliyoorodheshwa kwenye Muafaka wa Maelewano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Alipendekeza kuwa kongamano hiilo liwe sawa na lile kujadili marekebisho ya Katiba lililofanyika katika ukumbi wa Bomas mnamo 2005, mkutano ambao ulijumuisha wadau wote.

“Kamati ya BBI inapasa kuendesha shughuli zake kwa njia ambayo haitaonekana kama inaendesha mpango wa watu wawili, kwani hii ni hatari. Itakuwaje ikiwa mmoja wao atajiondoa? Bw Mudavadi akauliza alipohojiwa na wanahabari Jumatano asubuhi.

Akaongeza: “Kamati ya BBI inafaa kukumbatia mfumo wa Bomas kwa kuandaa mazungumzo yanayoshirikisha wadau wote kama ilivyofanyika katika Kongamano la Bomas lililoongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya marekebisho ya katiba (CRC) mwanasheria Profesa Yash Pal Ghai.

Bw Mudavadi alikariri kuwa chama chake cha ANC kinaunga mkono marekebisho ya Katiba lakini mchakato huo unapasa kujuisha Wakenya wa matabaka mbalimbali.

Kamati hiyo imekuwa ikikusanya maoni kutoka kwa Wakenya wa matabaka mbalimbali kuhusu namna ya kukabiliana na kero la migawanyiko ya kisiasa na fujo nchini kila baada ya uchaguzi mkuu. Pia imekuwa ikusanya mapendekezo ya umma kuhusu namna ya kumaliza ufisadi, ukabila na kuhimiza ujumuishaji wa wote katika serikali.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji inatarajiwa kukamilisha kazi yake mnamo Mei mwaka huu kwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Duru zasema kuwa kufikia sasa makundi na watu binafsi ambao wamewasilisha maoni na mapendekezo yao katika vikao vya kamati hiyo wamependekeza mabadiliko ya katiba kwa lengo la kugatuliwa kwa mamlaka ya kitengo cha afisi kuu kupitia kuundwa kwa vyeo vya Waziri Mkuu na manaibu wake wawili.

You can share this post!

KNBS yajitetea kuhusu Sh18 bilioni za sensa

Nairobi yaanza kupungukiwa na pato baada ya kupunguza ada...

adminleo