Ndani miaka 401 kwa kunajisi watoto wa mpenziwe
MASHIRIKA Na PETER MBURU
MWANAUME mmoja ambaye aliingia nchini Marekani kwa njia haramu amefungwa jela miaka 401, baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi watoto wawili.
Bw Macario Cerda wa miaka 39 alihukumiwa huko California katika makosa matatu ya kuwanajisi watoto wawili kwa nguvu mnamo 2009, 2010 na 2013.
Aidha, alihukumiwa katika kosa moja la kuteka nyara kwa nia ya kunajisi, makosa saba kuhusu matendo maovu kwa motto wa chini ya miaka 14 na moja la vitisho vya kijinai mnamo Januari 17.
Viongozi wa mashtaka walieleza korti kuwa mshtakiwa alikuwa na uhusiano na mamake mdhulumiwa, wakati mnamo Februari 26, 2013 alilazimisha mmoja wa wadhulumiwa kuingia katika gari lake na kumpeleka eneo fiche.
Mwanaume huyo anadaiwa kuendelea kumnajisi, huku akitishia kuwaumiza watu wa familia yake endapo wangesema. Ripoti za korti zilisema kuwa mamake mdhulumiwa alipigia polisi simu baada ya kumpigia mwanaye simu na kumsikia akipiga nduru.
Cerda baadaye alikamatwa na polisi na wakati wa uchunguzi ikabainika kuwa mdhulumiwa alinajisiwa alipokuwa motto, mnamo 2010.
Mdhulumiwa alipata mimba na kuzaa kutokana na tendo hilo, viongozi wa mashtaka wakasema.
Dadake mdogo mdhulumiwa aidha alimlaumu mshtakiwa kuwa aliwahi kumnajisi mnamo 2009, alipokuwa motto mchanga.
Aidha, alipatikana kuwa na vifungo vya mbeleni kuhusu vita vya kinyumbani na vitisho vya kijinai kwa mamake watoto hao.
Wakati huo, Cerda alitimuliwa US, lakini akarejea miezi mitano baadaye ambapo alitekeleza uovu huu, korti ikaelezwa.
Baada ya maombi kutoka kwa motto mmoja, korti ilikataa kumtimua tena jamaa huyo, na badala yake kumpa kichapo cha kifungo, kwa hofu kuwa angerejea tena.
“Hii familia haitaishi maisha yote kwa hofu kuwa Cerda atakuja kuwavamia, atahudumu siku zilizosalia za maisha yake katika jela la California,” korti ikaamua.