Makala

Mikakati ya Kaunti ya Kisumu kufagia magenge ya wahalifu

Na DOMINIC OMBOK November 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MENEJA wa Jiji la Kisumu Abala Wanga ametoa onyo kali kwa magenge yanayohangaisha watu jijini humo.

Bw Abala ametangaza kuwepo kwa mikakati ya kukabili magenge na kurejesha hali ya usalama.

Haya yanajiri baada ya kukithiri kwa mashambulizi dhidi ya wakazi na kusababisha maafa, majeruhi na kiwewe.

Makundi haya uhalifu yanayojumuisha vijana wa umri kati ya 12 na 30 husumbua wakazi wa Obunga, Manyatta, Nyalenda, Kibos, Kondele na Bandani.

Isitoshe, onyo la asasi za usalama Kisumu limeelekezwa hata kwa wazazi wa vijana wanachama wa magenge hayo.

“Iwapo unajua kuwa mwana wako anazua vurugu mitaani, mchimbie kaburi. Hatuwezi kuacha jiji ligeuzwe kuwa la uhalifu,” akafoka.

Alitangaza kuundwa kwa kikosi maalum cha walinda usalama wenye jukumu la kutambua na kuwakamata wahalifu.

“Tutawafuata hadi mafichoni kuwakamata. Tutaingia nyumba kwa nyumba na kuwashika. Tunaweza kukosa muda wa kuwapeleka katika kituo cha polisi kupata bondi ya Sh10,000,” akasema

“Na msiniambie kuhusu mauaji ya kikatili kwa sababu hawa, wanawaua watu,” aliongeza.

Meneja huyo wa jiji alisifu maafisa wa polisi kwa kuwakamata baadhi ya washukiwa hivi maajuzi.

 Mnamo Jumatano, Msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Kondele, Daniel Ogechi aliongoza oparesheni iliyoishia kwa kutiwa mbaroni kwa mshukiwa wa ujambazi Hillary Otieno Odera maarufu “Gonza.”

Odera alipatikana katika nyumba yake ya kukodi akiwa na bastola bandia.

Uchunguzi zaidi ulisaidia polisi kunasa mshukiwa mwingine Charles Otieno Otieno kwa lakabu “Baba Farouk”, mwenye umri wa miaka 24.

Alikamatwa akiwa mafichoni eneo la Kunya ambapo alipatikana na bangi, nyundo na jozi mbili za makasi.

Wote walifikishwa kizimbani na kushtakiwa huku bidhaa zilizopatikana zikihifadhiwa kuwa ithibati uchunguzi ukiendelea.

“Tutaendelea kuwakamata na kuwashtaki wahalifu,” Bw Ogechi alisisitiza.

Kamishna wa Kisumu Benson Laparmorijo alifichua baadhi ya mikakati ambayo wametekeleza kuangazia hali ya ukosefu wa usalama eneo hilo.

“Mbali na kuweka kafyu katika maeneo yaliyoathiriwa, tumezidisha doria kuanzia saa mbili usiku hadi mapema asubuhi,” alisema Bw Leparmorijo.

Alieleza kuwa kafyu inalenga kudhibiti watu wasitembee nyakati ambazo wahalifu wanashambulia wakazi, mpango ambao unaziba mianya ya kuchochea shughuli za uhalifu.

Oparesheni hizo zinahusisha maafisa wa polisi, vikosi vya usalama katika jamii, na vitengo maalum kuhakikishia wakazi usalama na kutibua njama za magenge hayo.

Vile vile, kamishna alisisitiza kuwa ushirikiano huo umekuwa na manufaa kwani wameweza kutambua maeneo hatari na kupata maelezo muhimu ya kuwezesha kukamatwa kwa wahalifu.

“Ushirikiano na umma ni wa maana sana.Tunawahimiza wakazi kutoa taarifa za matukio ya kutiliwa shaka kwa idara ya usalama,” alisihi Bw Leparmorijo.

 Kuweka thabiti mikakati hii, Kamati ya Usalama Kaunti ya Kisumu inatafuta suluhu ya kudumu.

Suluhu hizo zinahusisha uwezeshaji wa vijana kukabili ukosefu wa ajira.

Uhaba wa kazi ni kichocheo kikubwa cha usajili wa wahalifu katika magenge.

Zaidi ya hayo, kuna mipango ya kukita taa mitaani pamoja na kamera za usalama katika maeneo ambapo uhalifu umekithiri.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan