• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Washukiwa wa shambulizi la Garissa kujitetea Machi 21

Washukiwa wa shambulizi la Garissa kujitetea Machi 21

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA watano wa ugaidi wa shambulizi la Chuo Kikuu cha Garissa waliopatikana na hatia ya kuwaua wanafunzi 144 wa chuo kikuu cha Garissa miaka minne iliyopita wataanza kujitetea Machi 21.

Hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi alisema upande wa mashtaka unaoongozwa na wakili wa Serikali Bw Duncan Ondimu umewasilisha ushahidi unaowahusisha washtakiwa hao na shambulizi hilo.

Waliopatikana wako na kesi ya kujibu ni raia wa Tanzania Rashid Charles Mberesero na Wakenya Mohammed Ali Abikar, Hassan Edin Hassan na Osman Abdi Dagane.

Akiomba mahakama iwapate na hatia Bw Ondimu alimweleza hakimu. “ Nimewasilisha ushahidi unaothibitisha kinanga ubanga jinsi washtakiwa hawa walivyowasiliana kwa simu na magaidi waliotekeleza shambulizi hilo.”

Bw Ondimu aliyeongoza kesi hiyo akisaidiwa na Bi Carol Sigei alisema mashahidi aliowasilisha walielezea washtakiwa walivyohusika.

Hakimu alielezewa majukumu waliyotekeleza washtakiwa kabla ya shambulizi lililopelekea jumla ya watu 152 kufariki.

“Ushahidi tuliowasilisha umewahusisha washtakiwa wote katika mauaji hayo yaliyopelekea wanafunzi 144 kufa , maafisa wa kijeshi (KDF) Peter Chege, Solomon Obudo na Bernard Torikei, Afisa wa Polisi Peter Masinde na walinzi wawili Mohamed Hassan na Abdirizak Issak,” alisema Bi Sigei.

Lakini wakili Mbugua Mureithi anayewatetea washukiwa hao aliomba mahakama iwaachilie huru akisema “hakuna hata chembe ya ushahidi inayowahusisha wateja wake na shambulizi hilo ila mawasiliano tu kwa njia ya simu.”

Bw Mbugua alisema washtakiwa hao hawakuwa Garissa siku hiyo ya shambulizi na kwamba Mberesero alikuwa ametembelea rafiki mjini Garissa aliposhikwa.

“Hassan Edin Hassan alishikwa mjini Mandera umbali wa kilomita 700 na maafisa wa Kijeshi na kudaiwa alishiriki. Hakuna ushahidi wowote wa kumuhusisha na tukio hilo,” alisema Mureithi.

Mahakama ilielezwa kwamba “ hakuna hata mmoja wa washukiwa hao watano alikuwa chuoni siku ya mashambulizi hayo ya Aprili 3, 2015 yaliyopelekea Wakenya wengi kupatwa na mshtuko mkuu.

“Ikiwa kile kinafanya DPP aseme amethibitisha kesi ni mawasiliano ya simu basi ni hatia kumiliki simu humu nchini,” alisema Bw Mureithi huku akiomba mahakama iwaachilie huru kwa vile hawakuhusika na shambulizi hilo.

Washukiwa hao wamekanusha mashtaka walihusika na shambulizi hilo.

Maombi yao ya kuachiliwa kwa dhamana yalikataliwa na Bw Andayi akisema “ adhabu kali inayowakondolea macho washtakiwa ni kishawishi chao kutoroka.”

Wakipatikana na hatia washtakiwa watahukumiwa kunyongwa.

You can share this post!

Mwongozo wa kununua bidhaa NYS ulikuwa na dosari, korti...

Wanaoshukiwa kumteka nyara Mwitaliano kusalia ndani

adminleo