Ithibati kwamba kuna uwiano kati ya nyimbo na mashairi
NYIMBO hufanana pakubwa na mashairi, hasa kimuundo. Kwa kuwa wimbo ni kipera kimojawapo cha utanzu wa ushairi simulizi, ni muhimu tujijuze zaidi kuhusu baadhi ya vigezo vinavyofanya kipera hiki kuainishwa kama ushairi. Makala haya yatafafanua zaidi kufanana kwa nyimbo na mashairi.
Kwanza, ushairi huwa na sehemu inayorudiwarudiwa au kiitikio katika mshororo wa mwisho wa kila ubeti. Nyimbo pia huwa na sehemu inayorudiwarudiwa ingawa hutokea kama ubeti mfupi unaorudiwa badala ya kila mshororo wa mwisho wa ubeti kama ilivyo katika ushairi.
Mashairi hupangwa katika vifungu vya mishororo mbalimbali ambavyo huitwa beti. Kila kifungu huwa na ujumbe wake tofauti tofauti. Nyimbo pia huwa na vifungu mbalimbali ambavyo hupitisha ujumbe tofauti wa wimbo huo. Katika nyimbo, vifungu hivi ambavyo hujengwa kwa mishororo mbalimbali huitwa stanza.
Mbali na hayo, mashairi huwa na mizani inayolingana katika mishororo ili kuyasaidia mashairi haya kukaririwa kwa mapigo yenye muwala fulani. Nyimbo pia huwa silabi au mizani iliyo na urari ili kuwezesha utungo huu kuwa na mapigo ya kimuziki na hivyo basi kuufanya wimbo kuwa na muwala maalumu unaousaidia wimbo kuimbika.
Isitoshe, mashairi huwa na vina vya kati na vina vya mwisho ambavyo husaidia katika ukariri wa mashairi hayo. Vina katika nyimbo hubainisha urari ili kuwezesha wimbo kuwa na mapigo sawa ya kimuziki na hivyo hufanikisha uimbaji wake.
Mashairi hutumia lugha ya mkato ili kusawazisha mizani na vina katika ushairi. Halikadhalika, nyimbo hutumia lugha ya mkato ili kuleta muwala na mapigo ya muziki katika wimbo husika.
Aidha, beti katika mashairi mara nyingi huwa na mishororo inayolingana. Baadhi ya nyimbo pia huweza kuwa na idadi sawa ya mistari katika stanza ili kuleta uwiano wakati wa uimbaji wa nyimbo husika.