Kimataifa

Kenya hamtaki Adani lakini sisi tutaendelea naye, Tanzania wasema

Na REUTERS, CHARLES WASONGA November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

DAR ES SALAAM, Tanzania

SIKU chache baada ya serikali ya Kenya kuzima mpango wa kutoa kandarasi kwa kampuni mbili za Adan Group, afisa mmoja mkuu wa bandari Tanzania amesema haitafuta kandarasi iliyoipa mwekezaji huyo.

Hii ni licha ya kwamba mwenyekiti na mmiliki wa Adani Group, Gautam Adani, kufunguliwa mashtaka nchini Amerika kwa tuhuma za ufisadi na ulaghai.

Adani alishtakiwa wiki jana na agizo la kumkamata kutolewa dhidi yake kwa kutoa hongo ya dola 265 milioni (Sh35 bilioni) kwa maafisa wa serikali ya India ilia apate zabuni katika sekta ya kawi.

Bilionea huyo amekana tuhuma hizo.

Mnamo Mei mwaka huu, Tanzania ilitia saini mkataba na kampuni ya Adani Port, mojawapo ya matawi ya kampuni kubwa ya Adani Group, kusimamia eneo la kupakia makonteina katika bandari ya Dar es Salaam.

Mkataba huo ni wa kipindi cha miaka 30.

Adani Port pia ilikubaliana na Tanzania kununua asilimia 95 ya hisa katika kampuni ya Tanzania International Container Terminal Services kwa gharama ya dola milioni 95 za Amerika (Sh12.2 bilioni).

“Hatuna shida na mtu yeyote. Kila kitu tunachofanya ni kulingana na sheria zetu na makubaliano,” Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Bandari Tanzania Plasduce Mbossa akaambia shirika la habari la Reuters Jumanne jioni.

Alisema hayo alipoulizwa kuhusu hatima ya kandarasi hizo kwa misingi kuwa Adani ameshtakiwa kwa ufisadi nchini Amerika.

“Kwa kandarasi zetu, hatuna madai kama hayo (ya maovu kutendeka). Ikiwa kuna watu wanaochukua hatua basi wanafanya hivyo kutokana na sababu zao wenyewe,” Bw Mbossa akaeleza.

Mnamo Alhamisi wiki jana Rais wa Kenya William Ruto alifutilia mbali mkataba kati ya kampuni ya Adani Energy Solutions na kampuni ya umeme KETRACO ya kujenga nyaya za kusambaza umeme sehemu mbalimbali nchini.

Kampuni hiyo ilitarajiwa kutumia Sh96.7 bilioni kufanikisha mradi huo.

Aidha, alizima mpango wa utoaji kandarasi kwa kampuni ya Adani Airport kufanya upanuzi wa uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKAI) na kusimamia uwanja huo kwa miaka 30.

Adani Airports ilitarajiwa kutumia Sh277 bilioni kugharamia mradi huo.