Makala

Himizo serikali ifanye hima kukabili kero ya panya na konokono katika mashamba ya mpunga Kirinyaga

Na LABAAN SHABAAN November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKULIMA wa mpunga katika Kaunti ya Kirinyaga wanaomba serikali ifanye hima katika kubuni mikakati ya kumaliza vimelea wanaovamia mashamba yao na kuwasababishia hasara.

Mmmoja wa wakulima Lucy Njoki anasamilia anavyotaabika baada ya panya na konokono kuvamia shamba lake lililoko Mwea.

Si mara moja amefikiria kuacha kilimo hiki baada ya wanyama hawa kuwa kero. Ila kila siku anajipa nguvu akiamini suluhu itapatikana haraka.

“Mwaka huu tumepata changamoto nyingi sana kama vile konokono na panya. Wanakula mimea ya mchele na unaweza kukuta ekari imebaki bila kitu,” alilalama Bi Njoki katika mahojiano na Taifa Leo.

Wakati mwingi huwa wanavamia shamba tunapohamisha mpunga kutoka katika vitalu na kupandikiza shambani,” akaongeza akisema huwabidi kupanda tena kurejesha mimea shambani, hali ambayo huwapa hasara kubwa.

Mkulima wa Mpunga katika mradi wa Mwea Lucy Njoki. Picha|Labaan Shabaan

Kama wakulima wengine, Bi Njoki anaomba serikali ifanye hima kuunda mikakati ya kushughulikia changamoto zao.

Wanateta kuwa kununua ama kubuni dawa za kumaliza wanyama hawa kumeongeza gharama ya kilimo zaidi.

“Huwa tunatumia dawa lita moja kunyunyizia shambani ili kuua konokono,” alieleza akifichua hawajapata dawa mahususi kukabili panya.

“Ili kuua panya wakulima hujiundia dawa kwa kuchanganya nyanya, simiti na pilipili na kumwaga katika mashimo ya panya shambani.”

Wakulima wakausha mavuno ya mpunga ili kupata mchele. Picha|Labaan Shabaan

Serikali kuunda jopokazi

Kuangazia matatizo haya, serikali inapanga kuunda jopokazi la kudhibiti wanyama hawa.

 Jopokazi hilo litajumuisha wanachama kutoka Wizara ya Kilimo na wengine kutoka Kaunti ya Kirinyaga.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa Maji, Unyunyuzaji na Usafi wa Mazingira, Eric Mugaa alisema: “Kasi ambayo panya hao wanaongezeka katika shamba na kuharibu mpunga inatia wasiwasi. Panya wanaathiri uzalishaji wa mpunga na mitego haitasaidia, lazima tafute suluhu ya kudumu kwa tatizo hili.”

Mkulima aonyesha mmea wa mpunga shambani Mwea. Picha|Labaan Shabaan

Mikakati hii inalenga kusaidia wakulima kupata manufaa makubwa kutokana na kilimo cha mpunga.

Mipango hii mipya ya serikali ilipata pingamizi kutoka kwa umma baada ya Wakenya kuona ikiwa njama ya kuiba mali ya umma.

“Tatizo hili halihitaji jopokazi kukabiliana nalo. Suluhu ni wataalamu na viongozi wa serikali wa wizara husika wafanya kazi yao,” alisema Mkenya mmoja katika mitandao ya kijamii.

Wakulima wanalalamika kwamba, hata mitego iliyowekwa kwenye mashamba haisaidii.

Wanaamini ni serikali za kitaifa na kaunti pekee ndizo zinaweza kukabiliana na tishio la panya.

Bw Mugaa alisema wakulima wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa mpunga na wanapaswa kusaidiwa.

Mradi huo, mkubwa zaidi nchini Kenya unachangia asilimia 80 ya mchele unaotumiwa kitaifa.

Shamba la mpunga Mwea, Kaunti ya Kirinyaga. Picha|Labaan Shabaan