HabariSiasa

Uteuzi wa Matiang'i tumbojoto kwa wandani wa Ruto

January 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

UTEUZI wa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kusimamia kamati ya maendeleo na utekelezaji wa miradi ya serikali ya kitaifa, umeibua hisia kali miongoni mwa Wakenya.

Uteuzi huo ulichukuliwa na wengi kama wa kumpandisha hadhi Bw Matiang’i na njama ya kupunguza majukumu ya Naibu Rais William Ruto. Jumatano, washirika wa Bw Ruto walitaka kujua majukumu ambayo atakuwa akitekeleza serikalini kufuatia uteuzi wa Dkt Matiang’i.

Mbunge wa Keiyo Kusini, David Rono na Seneta wa Nandi Samsom Cherargei walisema japo Rais ana haki ya kupanga serikali yake atakavyo, haifai waziri kusimamia mawaziri wenzake. “Swali kubwa ni, majukumu ya Ruto yatakuwa gani katika mpangilio huu mpya?” alihoji Bw Rono.

Bw Charargei alisema uteuzi huo haufai kutumiwa kama leseni ya kumhujumu Bw Ruto.

Waliomtetea Rais Kenyatta walisema hakufanya makosa yoyote huku wengine wakisema ilionyesha Bw Ruto hatakikani serikalini. Mwanaharati wa kisiasa Tony Gachoka ambaye amekuwa akimkosoa vikali Bw Ruto, alisema kumteua Bw Matiang’i kusimamia kamati ya taifa ya maendeleo na mawasiliano ya baraza la mawaziri ni hatua ya kwanza ya kumfanya Bw Ruto kueleza anakotoa pesa anazotoa katika harambee kote nchini.

Seneta wa Kaunti ya Narok, Ledama Ole Kina alishangazwa na hatua ya rais ya kumpandisha hadhi Dkt Matiang’i na kumfananisha waziri huyo na waziri mkuu.

“Kwa hivyo tuko na waziri mkuu Kenya au ni mkuu wa mawaziri? Hizi siasa za urithi zimeanza kuwa mbaya,” alisema Bw Ole Kina kwenye Twitter.

Alikosoa uteuzi huo akisema Dkt Matiang’i hajaondolewa lawama kuhusu sakata ya ardhi ya shule ya Ruaraka na amekuwa akikaidi maagizo ya mahakama. Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Profesa Edward Kisiangani, uteuzi wa Dkt Matiang’i utasaidia kulinda mali ya umma, kupigana na ufisadi na kufuatilia miradi ya serikali. “ Ili kutimiza malengo haya, anahitaji watumishi wa umma na viongozi wa kisiasa waliojitolea,” alisema msomi huyo.

Kuna wanaohisi kwamba Rais alimkabidhi Bw Matiang’i mamlaka hayo ili kumzima Bw Ruto.

“Ruto ni mkali lakini sasa lazima awe mjanja zaidi kwa sababu Matiang’i pia ni mkali na iwapo Naibu Rais atavuka mipaka, waziri atamwekea breki na kutakuwa na mzozo. Ikiwa kuna mtu anayeweza kumwangalia machoni Dkt Ruto na kumkosoa, basi ni Dkt Fred Matiang’i,” aliandika Bw Benji Ndolo, mwanaharakati na mdadisi wa siasa.

Kulingana na mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria, uteuzi wa Dkt Matiang’i ni mwanzo wa marekebisho ya katiba nchini kabla ya kura ya maamuzi.

Mbunge huyo alisema Dkt Matiang’i atamsaidia Rais Kenyatta na Dkt Ruto kuendesha serikali.

“Hivi ndivyo nilivyokuwa nikifikiria nilipopendekeza wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake wawili wateuliwe kusaidia rais na naibu wake katika majukumu yao muhimu,” alisema Bw Kuria.

Naye mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Homabay Gladys Wanga na kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi walisema Rais hakukiuka katiba kwa kumpa Dkt Matiang’i mamlaka makuu. Jana, Dkt Ruto alisafiri hadi Mombasa alipoungana na Rais Kenyatta na viongozi wa chama cha Jubilee bungeni kwa mkutano na chakula cha mchana.