Habari Mseto

Mjukuu wa Moi alegeza msimamo, akubali kuwajibikia masuala ya ulezi wa wanawe

Na JOSEPH OPENDA November 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MJUKUU wa aliyekuwa Rais Daniel Moi, Collins Kibet, amelegeza msimamo wake kuhusu malezi ya watoto wake na kupendekeza hatua za kuhakikisha watoto hao wananufaika na mali ya familia yake.

Hii inafuatia mzozo wa muda mrefu wa kisheria kuhusu madai yake ya kupuuza majukumu yake kama mzazi.

Bw Kibet ambaye anakabiliwa na kesi ya kutotii amri ya mahakama iliyotolewa Juni 2022, aliwasilisha mapendekezo Novemba 27 ya kuwatunza watoto hao wawili na akaeleza nia yake ya kuwatambulisha watoto hao, ili  wanufaike na baadhi ya manufaa anayostahili kutokana na uhusiano wake na familia ya Moi.

Ameahidi kuwasajili katika Shule maarufu ya Kabarak na kulipia gharama zao za matibabu kupitia Kituo cha Huduma za Afya cha Kabarak.
Mjukuu huyo wa Moi anataka pia aruhusiwe kuwaona watoto pamoja na kuwa nao wakati wa likizo za shule.

“Mshtakiwa atahakikisha watoto wanasajiliwa katika Shule ya Kabarak kwa elimu yao. Atashughulikia mahitaji ya matibabu ya watoto kupitia Kituo cha Huduma za Afya cha Kabarak na wazazi wote wawili wawe na uwezo wa kuwafikia watoto wakati wa likizo za shule,” akasema Bw Kibet kwenye mawasilisho mahakamani.

Bw Kibet pia anataka mama wa watoto hao Gladys Jeruto Tagi,  kudumisha malezi halisi ya watoto. Anapendekeza wazazi wote wawili wachangie gharama za chakula, mavazi na burudani wanapokuwa na watoto.

Haya yanajiri baada ya mahakama kumwita Bw Kibet aeleze ni kwa nini asiadhibiwe kwa kukosa kutii amri ya kumtaka kutoa Sh 1.6 milioni kila mwaka kwa mahitaji ya watoto wake, ikiwa ni pamoja na elimu, matibabu na burudani.

Maagizo hayo yalitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Bw Benjamin Limo,  baada ya Bi Tagi kumshutumu Bw Kibet kwa kupuuza majukumu yake kama mzazi.

Mzozo huo uliongezeka na kusababisha Bw Kibet kukamatwa na kufungwa jela kwa wiki moja mnamo Septemba. Hukumu hiyo iliondolewa baadaye.

Katika utetezi wake, Bw Kibet ambaye ni mwana wa Jonathan Toroitich, alijitaja kuwa maskini na anayekumbwa na msongo wa mawazo.Alisema hana kazi, hana mahali pa kuishi na anategemea wasamaria wema.

Alisema matatizo yake yalianza baada ya kupoteza watu wa karibu wa familia yake akiwemo mama yake, baba yake, babu na shangazi yake ambao walikuwa wakimjali.

Hakimu Mwandamizi, Bw Kipkurui Kibet,  alimwagiza Bi Tagi kujibu ombi la Kibet kabla ya kesi hiyo kutajwa Januari 15, 2025.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA