Kimataifa

Rais Biden azima mashtaka ya mwanawe Hunter Biden akielekea kuondoka afisini

Na CHARLES WASONGA, REUTERS December 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WASHINGTON, Amerika

RAIS wa Amerika Joe Biden alisema Jumapili kuwa amemsamehe mwanawe wa kiume, Hunter Biden, aliyeshtakiwa kwa kutoa taarifa za uwongo, kumiliki bunduki kinyume cha sheria na kutolipa ushuru.

“Leo (Jumapili) nilitia saini hati ya msamaha kwa mwanangu Hunter. Tangu nilipoingia mamlakani nilisema sitaingilia uamuzi wa Idara ya Mashtaka na nilizingatia msimamo huo hata nikitazama mwanangu akikosa kutendewa haki kwa kushtakiwa,” akasema kwenye taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House.

Ikulu ya White House ilikuwa imesema kila mara kwamba Biden hangemsamehe wala kuzima mashtaka dhidi ya mwanawe, ambaye anaendelea kurejelea maisha ya kawaida baada ya kutekwa na matumizi ya mihadarati.

Hunter Biden alishambuliwa, kwa maneno, na wanachama wa Republican akiwemo Rais mteule Donald Trump.

“Hamna mtu mwenye akili timamu anayeweza kukagua kesi dhidi ya Hunter na kuamini vingine isipokuwa kwamba Hunter alilengwa kwa sababu ni mwanangu,” Biden akasema.

Hunter Biden alitarajiwa kusomewa kwa kosa la kutoa taarifa za uwongo na kumiliki bunduki bila kinyume cha sheria.

Mnamo Septemba mwaka huu alipatikana na hatia ya kosa la kufeli kulipa ushuru wa kima cha dola 1.4 milioni (Sh180 milioni) huku akitumia pesa kwa anasa kama vile dawa za kulevya, makahaba na bidhaa za starehe.

Hunter Biden alitarajiwa kusomewa hukumu kuhusiana na kesi hiyo mnamo Desemba 19.