EACC inachunguza ufisadi wa Sh2 bilioni katika kaunti sita za Bonde la Ufa
TUME ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) inachunguza ufisadi wa Sh2 bilioni katika kaunti sita za Bonde la Ufa.
Wapelelezi hawa wanalenga viongozi tofauti wa Kaunti za Nakuru, Bomet, Baringo, Kericho, Pokot Magharibi na Samburu ambapo mikataba imeibua maswali jinsi pesa za umma zimefujwa.
Haya ni kwa mujibu wa meneja wa EACC kanda ya Bonde la Ufa Kusini Ignatius Wekesa.
“Uchunguzi ukikamilika, hatua zinazofaa zitachukuliwa,” akasema.
EACC inapeleleza maafisa 18 wa Kaunti ya Bomet.
Serikali ya Gavana Hillary Barchok inahusishwa na wizi wa Sh1.573 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023.
Tume hii imethibitisha kuwa mawaziri watatu wa kaunti na maafisa wakuu wawili ni miongoni mwa maafisa wanaowekwa kwenye mizani.
Wanatuhumiwa kwa kuingilia mchakato wa zabuni na kufyonza pesa za umma kupitia kampuni wanazomiliki ama zinazomilikiwa na familia zao.
“Ni vyema bunge la kaunti liliwatimua mawaziri watatu muda mrefu kabla ya EACC kuchukua hatua. Tunataka Gavana na Bodi ya Utumishi wa Umma katika kaunti kuwachukulia hatua waliotajwa katika uchunguzi,” akasema Bw Stephen Changmorik, Diwani wa Longisa.
Washukiwa hawa wamenunua mali maeneo ya Kericho, Eldoret na Nairobi huku wengine wakitumia pesa hizo kujenga majengo ya kibiashara na makazi Bomet, Narok, Kericho na Nairobi.
Katika Kaunti ya Nakuru, maafisa 14 wa serikali ya Gavana Susan Kihika wanamulikwa kuhusiana na sakata ya zabuni ya Sh27 milioni za kununua vifaa vya michezo katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024.
Washukiwa hawa wamehojiwa na kusukumwa kuandikisha ripoti kuhusu tuhuma zinazowakabili.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa maafisa wakuu wa kaunti walikula njama ya kununua vifaa duni vya michezo kwa bei ya juu sana.
Inadaiwa kandarasi zilitolewa kwa kampuni wanazomiliki wao, familia zao ama kampuni za kisiri.
Wapelelezi hawa pia wanachunguza maafisa wa Bunge la Kaunti ya Baringo kuhusiana na madai ya ubadhirifu wa pesa za umma kupitia ulipaji wa marupurupu kinyume cha sheria.
Kulingana na EACC, bila kuzingatia sheria, madiwani walibuni angalau kamati sita za ziada katika bunge na kuzitumia kujilimbikizia marupurupu.
Hali ni hiyo hiyo katika Kaunti ya Kericho ambapo kampuni saba zilinyonya Sh39 milioni za gatuzi hilo.
Kampuni hizo zinashukiwa kunufaika kwa kandarasi za miradi ya kurembesha manispaa za Kericho na Litein licha ya kutokuwa na uwezo wa kufanikisha miradi hii katika mwaka wa kifedha uliopita.
Katika Kaunti ya Pokot Magharibi, wapelelezi wa EACC wamekamilisha uchunguzi kuhusiana na ubadhirifu wa pesa za kima cha Sh296 milioni na kuwakamata washukiwa wawili.
Tume hiyo ilibaini fedha hizo zilikusudiwa kutumika kuwa basari za wanafunzi wa familia maskini Pokot Magharibi.
Kamati ya seneti vile vile imebaini kuwa Sh390 milioni zimetumiwa vibaya katika Kaunti ya Samburu na kuelekeza uchunguzi wa kina ufanywe.
Kamati ya Fedha za Umma katika Kaunti (CPAC) inayoongozwa na Seneta Moses Kajwang’ imekemea serikali ya Gavana Lati Lelelit kwa kuwaajiri wafanyakazi bila mikataba na kubuni afisi tofauti bila kufuata sheria.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan