Mzee alilia haki baada ya Sh1.1 milioni kuporwa na wakora wa kubadilisha laini za simu
TESO KASKAZINI
MZEE kutoka Kijiji cha Kaeset eneo Bunge la Teso Kaskazini ameporwa takribani zaidi ya Sh1 milioni baada ya kuhadaiwa kuuziwa laini mpya ya simu.
Mzee Camil Pius Etyang alieleza kwamba vijana watatu asiowajua walifika kwake alasiri na kutaka kumuuzia bidhaa za jikoni na kumbadilishia laini yake ya Safaricom.
Baada ya mazungumzo, Camil alipendezwa na bidhaa licha ya wao kutofautiana kwa bei. Wauzaji vile vile walimshawishi kubadilishiwa laini ili apewe mpya.
Walichukua simu ya Camil na kutoa laini yake na kuweka laini mpya. Baada ya muda mfupi walikuwa wamebadilisha laini bila yeye kujua na kutoa pesa.
Wahalifu hao walipotea mara moja baada ya kufaulu katika njama yao.
Baada ya kugundua kwamba ameporwa, Camil alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Malaba.
Kulingana na ripoti aliyopeana katika kituo cha polisi, wahalifu walifaulu kutoa Sh1,100,000 kutoka katika akaunti yake ya KCB, Sh2,000 kutoka kwa Mpesa na Sh7,000 kutoka kwa Mshwari.
Kisa hiki kimemuacha Mzee Camil na kilio huku polisi wakianzisha uchunguzi.