Habari Mseto

Makachero wachunguza mkulima wa miraa kuzikwa kisiri na binamu zake

Na GEORGE MUNENE December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAKACHERO wanaendelea kufanya uchunguzi kuhusu kisa ambacho mkulima wa miraa aliuawa na mwili wake ukapatikana umezikwa kwenye kaburi la kina kifupi katika kijiji cha Kivwe, Kaunti ya Embu.

Mkulima huyo Apodia Njuki Njoka, 32, alitoweka mnamo Novemba 24 lakini mnamo Disemba 2, mwili wake ambao ulikuwa na majeraha mabaya ulipatikana umezikwa kwenye boma la binamu wake wawili.

Wanakijiji ambao walikuwa na hamaki waliwafurusha binamu hao kutoka nyumba zao na kudai walihusika na mauti hayo kisha kumvamia mmoja wao.

Mmoja wao aliokolewa na polisi na akakimbizwa hadi Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Siakago kabla ya kuhamishwa hadi hospitali ya rufaa ya Embu akiwa katika hali mbaya kiafya.

Kwa mujibu wa familia, marehemu Njoka alitoweka nyumbani wiki moja iliyopita. Familia yake ilianza kumtafuta kwenye vichaka na maeneo jirani lakini hawakumpata.

Mnamo Jumapili, baada ya kupigwa jeki na wakazi, familia hiyo ilipata kaburi ambalo ndilo lilikuwa limechimbwa na wakashuku Bw Njoka alikuwa amezikwa hapo.

Hapo ndipo waliwafurusha binamu hao kutoka nyumba zao wakawaangushia kipigo kikali na kutisha kuwaua wasipowaambia wakitaka ukweli.

Kuona mambo yanawaendea vibaya, ndugu hao walifunguka na kusema walimzika Bw Njoka kwenye kaburi hilo na wakakiri kuwa walihusika na mauaji yake.

Wakazi waliendelea kuwapiga na kuwajeruhi vibaya huku wakilaani mauaji hayo. Polisi kutoka Siakago walifika na kuwaokoa wawili hao kisha kuwapeleka katika Hospitali ya Siakago ambapo mmoja wao aliaga dunia.

Inahofiwa kuwa Bw Njoka aliuawa na kuzikwa kisiri kutokana na mzozo wa shamba.

Phrisnah Wanjue, dadake marehemu  alisema kuwa nduguye aliuawa kwa njia ya kikatili na akasisitiza kuwa lazima wapate haki.

“Tunashuku aliuawa kwa sababu alikuwa na shamba kubwa la miraa karibu na boma la washukiwa ambao walikuwa wakilimezea mate. Walitaka kuchukua shamba hilo kiharamu ndiposa walikuwa wakitaka kulichukua,” akasema Bi Wanjue.

Mauti ya Bw Njoka, baba wa watoto wanne, wote wakiwa mapacha kumeiacha familia, wakazi na marafiki zake wakiwa na mshtuko.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mbeere Kaskazini Eric Yego alisema makachero wanaendelea kuchunguza mauti hayo na kutoa wito kwa familia wake wawe watulivu na wanakijiji wadumishe amani.

“DCI wamechukua usukani na wanasuburi mwili huo ufukuliwe kisha hapa ndipo watafahamu jinsi ambavyo marehemu aliuawa. Hili ni suala ambalo lipo mikononi mwetu na tunatoa wito kuwe na utulivu,” akasema Bw Yego.