Makala

Wakenya wakodolea msimu mgumu wa sherehe bei za bidhaa muhimu zikianza kupanda

Na BENSON MATHEKA December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

HUENDA Wakenya wakasubiri kwa muda kuona uthabiti katika gharama ya maisha huku bei za bidhaa muhimu zikipanda tena na kufanya maisha kuwa magumu.

Mfumuko wa bei nchini Kenya ulipanda hadi asilimia 2.8 mwezi wa Novemba 2024, kutoka asilimia 2.7 iliyorekodiwa mwezi Oktoba 2024, ongezeko ambalo limechangiwa na kupanda kwa bei za bidhaa zinazotumiwa kila siku.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Kitaifa la Takwimu Kenya (KNBS), kuhusu viwango vya bei, kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji visivyo na vileo, ndiyo sababu kuu za mfumuko wa bei mwezi jana.

“Kupanda kwa gharama ya maisha kulichangiwa zaidi na kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji visivyo na vileo Novemba 2024 ikilinganishwa na Novemba 2023,” ilisema sehemu ya ripoti ya KNBS.

Mfumuko wa bei wa mwezi hadi mwezi ulikuwa asilimia 0.3 Novemba 2024. Hata hivyo, bei za bidhaa katika sekta ya uchukuzi zinaripotiwa kupungua kwa asilimia 1.1 Novemba mwaka huu ikilinganishwa na Novemba 2023.

Kwa kipimo cha mwezi kwa mwezi, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 0.3 ikilinganishwa na asilimia 0.2 mwezi Oktoba, KNBS ilisema katika ripoti yake.

Kenya inalenga kiwango cha mfumuko wa bei cha kati ya asilimia 2.5 na asilimia 7.5 katika muda wa kati.

Kulingana na ripoti hiyo, bidhaa muhimu za vyakula kama vile mafuta ya kupikia zilipanda kwa asilimia 3.1, sukari kwa asilimia 5.3, na unga wa mahindi akwa asilimia 5.1.

Hii inaashiria kuwa msimu wa sherehe za mwisho wa mwaka utakuwa mgumu kwa Wakenya hasa kufuatia kupanda kwa bei za bidhaa muhimu ambazo zilikuwa zimeshuka kufikia mwisho wa Oktoba 2024.