Habari Mseto

SGR ya Naivasha kuzinduliwa Juni

January 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

AWAMU ya pili ya reli ya kisasa (SGR) itazinduliwa Juni mwaka huu, Shirika la Reli Nchini (KR) limetangaza.

Kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter, usimamizi wa shirika hilo umesema kuwa kufikia sasa kiwango cha kukamilika kwa ujenzi huo kimefikia asilimia 88.

“Ujenzi wa awamu ya pili ya SGR kutoka Nairobi hadi Naivasha unaendelea ulivyopangwa. Asilimia 88 ya kazi imekamilika kuashiria kuwa uzinduzi wake utafanyika Juni, 2019 ilivyoratibiwa,” KR ikasema.

Kumekuwa na wasiwasi kwamba huenda mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya China Roads and Bridges Corporation (CRBC) usikamilike kufikia Juni mwaka huu kutokana na vuta nikuvute kuhusu ulipaji ridhaa kwa wenye ardhi iliyotwaliwa.

Hata hivyo, mnamo Desemba mwaka jana, kaimu mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Philip Mainga alitangaza kuwa ulipaji fidia umeanza na kawataka wamiliki kuondoka katika maeneo ya ujenzi wa reli hiyo.

Mzozo huo ulishamiri zaidi katika maeneo karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi, Embulbul na Ngong.

Katibu wa Wizara ya Uchukuzi, Paul Maringa jana alisema kuwa reli hiyo ya umbali wa kilomita 120 itazinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta wakati wa sherehe za Madaraka Dei.

“Mradi huu unaogharimu Sh150 bilioni unaelekea kukamilika na utazinduliwa na Rais Kenyatta mnamo Juni mosi mwaka huu. Masuala yote ya ulipaji fidia yametatuliwa na kazi inaendelea kukamilika kupitia ushirikiano wa mwanakandarasi, KR na Tume yaKitaifa ya Ardhi,” akasema.

Reli hiyo ambayo inapitia katika kaunti tano za Nairobi, Kajiado, Kiambu, Nakuru na Narok inatarajiwa kuchochea maendeleo mjini Naivasha na maeneo ya karibu.

Hata hivyo, kumekuwa na dukuduku kwamba huenda China ikakosa kutoa fedha za kugharamia ujenzi wa SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu na kisha kutoka Kisumu hadi Malaba.