Je, Ruto atafika kortini kutoa ushahidi dhidi ya mwanachuo?
SUALA gumu litakalozua mjadala mkali katika ni ikiwa Rais William Ruto atafika kortini kutoa ushahidi katika kesi ambapo mwanafunzi wa chuo kikuu ameshtakiwa kuchapisha habari za uongo kumhusu.
Kesi dhidi ya David Ooga Mokaya, mwanafunzi wa mwaka wa wanne katika Chuo Kikuu cha Moi, inavuma sasa nchini hasaa katika mitandao ya kijamii.
Hakimu mkazi Benmark Ekhubi alidokezewa na mawakili Ian Mutiso na Danstan Omari kwamba “kesi hii itakuwa ya kihistoria kwa vile wataomba Rais Ruto aagizwe afike kortini kutoa ushahidi na kuhojiwa vikali.”
Bw Ekhubi aliambiwa kwamba mawakili wapatao 21,000 wa chama cha wanasheria nchini (LSK) wamejitolea kumtetea Mokaya na watamhoji Rais Ruto kuhusu uhuru wa kusema na kujieleza kwa mujibu wa Katiba ya 2010.
“Suala ambalo tutamtaka Rais Ruto afafanue ni ikiwa akikosolewa ama akipingwa na mtu ni makosa ya jinai,” Bw Omari alieleza mahakama kwa waziwazi.
Bw Omari alieleza mahakama kwamba “swali ambalo Rais Ruto atajibu ni ikiwa ndiye alikuwa ndani ya jeneza lililokuwa linaburutwa ikiongozwa na maafisa wa kijeshi wakiwa wamejikwatua mavazi yao rasmi ya sherehe ama siye.”
Pia wakili huyo alisema atataka Rais Ruto aeleze ikiwa ndiye “alikuwa ndani ya jeneza hilo amewezaje fika kortini kutoa ushahidi?”
Mahakama iliambiwa kuwa hapo ndipo kizugumkuti kipo.
“Tutaonana naye ana kwa ana akijibu maswali kutoka kwetu.”
“Naomba upande wa mashtaka (DPP) umuepushie Rais Ruto kejeli na aibu kwa kutathmini upya kesi hii,” Bw Omari alisema.
Wakili huyo pamoja na Bw Mutiso walisema huenda kesi hii inasukumwa kisiasa ikizingatiwa kuwa Chuo Kikuu cha Moi kinakumbwa na matatizo makubwa ya usimamizi.
“Si jambo fiche kwamba Chuo Kikuu cha Moi kiko hali mahututi na wanafunzi wana hofu kuu ikiwa kitarejelea hali yake ya awali,” alieleza Bw Omari.
Wakili Omari alirudia kwamba itakuwa ni aibu kuu kwa Rais kufika kortini kueleza kuhusu suala hili la jeneza lililovishwa bendera ya Kenya na uhuru wa kusema.”
Omari alisema watawasiliana na DPP kuhusu kesi na kumtaka atathmini upya uamuzi huu wa kumfungulia mashtaka mwanafunzi huyu.
“Tangu Mokaya afikishwe kortini zaidi ya wiki tano, DPP hajamkabidhi nakala za ushahidi,” Bw Mutiso alieleza mahakama.
Wakili huyo alieleza masikitiko yake kwamba muda umeyoyoma na Mokaya hajapewa nakala za mashahidi ajiandae kujitetea.
“Tunaomba afisi ya DPP imkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi pamoja na ile ya Rais Ruto tujue amesema nini,” Bw Mutiso alisema.
Bw Omari alidokeza: “Tutahitaji kujua ikiwa DPP amewasiliana na Rais Ruto kujua kama atafika kortini kutoa ushahidi.”
Bw Omari alisema kesi za hapo awali ambapo watu walishtakiwa kwa kumuiga rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kulaghai wawekezaji kutoka ng’ambo ziliondolewa.
Pia kesi ambapo mfanyakazi wa hoteli alisambaza video ya Bw Kenyatta na Bw Raila Odinga wakitembea usiku wakati wa kafyu siku za mlipuko wa Covid-19 ilitamatishwa kwa sababu rais na waziri mkuu wa zamani wasingefika kortini kutoa ushahidi.
“Ni bayana hii kesi itatamatishwa tu,” Bw Omari alieleza korti.
Mawakili hao pia walisema polisi walitwaa simu na tarakilishi ya mshtakiwa na kuenda nazo na kufikia sasa hawajamrudishia.
“Mshtakiwa anatarajia kuhitimu Disemba hii na hawezi kujaza fomu katika harakati za kujiandaa kuhitimu. Simu na tarakilishi yake iko na taarifa muhimu atakazotumia kujaza fomu hizo. Sasa hawezi,” Bw Omari alisema.
Kiongozi wa mashtaka Virginia Kariuki aliomba kesi hiyo itajwe baada ya muda wa mwezi mmoja ndipo afisa anayeichunguza apate simu na tarakilishi hiyo kutoka kitengo cha uhalifu wa kimitandao.
Pia, Bi Kariuki alisema kesi hiyo haijasukumwa kisiasa akisema “DPP hafungulii mshukiwa mashtaka kwa misingi ya kisiasa ila anaongozwa na sheria.”
Akitoa uamuzi Bw Ekhubi alisema kuwa atasubiri uamuzi wa DPP kuhusu nakala za ushahidi na ikiwa atatathmini upya uamuzi wa kumshtaki Mokaya.
Kesi hiyo itatajwa Januari 28, 2025 kwa maagizo zaidi.