• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
Wanafunzi wavivu kunyimwa ufadhili wa masomo

Wanafunzi wavivu kunyimwa ufadhili wa masomo

NA KALUME KAZUNGU

WANAFUNZI wavivu waliopokea ufadhili wa kimasomo kutoka kwa serikali ya kaunti ya Lamu huenda wakapoteza nafasi zao iwapo hawatajitahidi kufanya vyema masomoni.

Wawakilishi wa Wadi katika bunge la Kaunti ya Lamu wanasema katu hawatavumilia kuona fedha za umma zikiendelea kutumiwa kuwafadhili wanafunzi wasiowajibika masomoni.

Kaunti ya Lamu mwaka huu ilitenga jumla ya Sh 127 milioni ili kufadhili elimu ya wanafunzi wa shule za sekondari, taasisi na vyuo vikuu kote Lamu.

Kaunti pia ilitangaza kuwafadhili wanafunzi wote ambao walipata alama 300 na zaidi kwenye mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE).

Wakizungumza na wanahabari nje ya majengo ya Bunge la Kaunti ya Lamu Ijumaa, madiwani hao aidha walisimama kidete kutangaza hali ya hatari kwa wanafunzi wasiowajibikia masomo yao.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kaunti ya Lamu, ambaye pia ni Mwakilishi wa Wadi ya Shela, Azhar Mbarak, madiwani hao walisema fedha za mfuko wa basari ya kaunti huwafadhili wanafunzi werevu pekee.

Bw Mbarak alisema kaunti haitamhurumia mwanafunzio atakayefadhiliwa na kisha kuanza kurekodi matokeo duni shuleni anakofadhiliwa.

Alisema iwapo mwanafunzi ataanguka masomo yake, kaunti itapunguza kiwango cha ufadhili au hata kukatiza kabisa ufadhili huo na kuelekeza nguvu zake katika kuwafadhili wanafunzi wenye bidii.

Aliwataka wazazi kuwaelekeza watoto wao katika njia inayostahili kwa kuwahimiza kutia bidii maishani.

“Elimu ndio ufunguo wa maisha. Hii ndiyo sababu tukaweka kipaumbele suala la elimu katika kaunti yetu. Tumetenga Sh 127 milioni za kufadhili elimu ya wanafunzi kote Lamu. Tumeafikia kufadhili wanafunzi wote waliopata alama 300 na zaidi kwenye mtihani wa KCPE.”

“Hii haimaanishi kwamba punde mwanafunzi utakapofadhiliwa basi usiwajibike masomoni. Lazima wadumishe rekodi zao za kufanya vyema. Ukianguka tutaishinikiza kaunti kufutilia mbali ufadhili wako wa kimasomo. Fedha zilizotengwa ni kwa minajioli ya wanafunzi werevu pekee,” akasema Bw Mbarak.

Naye Mwakilishi wa Wadi ya Kiunga ambaye pia ni Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Lamu, Abdalla Baabad, aliwahakikishia wanafunzi kutoka jamii ya walio wachache ya Waboni eneo la Basuba na wale wa kutoka jamii za wafugaji wa kuhamahama kwamba watapewa kipaumbele katika ufadhili huo wa kimasomo.

“Fedha za kutosha zimetengwa kufadhili elimu ya wanafunzi wetu hapa Lamu. Hii ni fursa nzuri ya wazazi kuwahimiza watoto wao kusoma. Tutahakikisha watoto kutoka jamii ya Waboni eneo la Basuba na wale wa jamii za wafugaji wanapokea ufadhili wa mbele katika mpango huo,” akasema Bw Baabad.

Naye Mwakilishi wa Wadi ya Witu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu katika Bunghe la Kaunti ya Lamu, Bw Jonathan Mketta, aliwataka wazazi kuwahimiza watoto wao kuzingatia elimu ili kuwawezesha kupata ujuzi utakaowasaidia kupata kazi kwenye mradi unaoendelea wa Bandari ya Lamu (LAPSSET).

You can share this post!

Chepng’etich aibuka bingwa wa Dubai Marathon

Wakili kutoka Uingereza aruhusiwa kuongoza mashtaka dhidi...

adminleo