Jamhuri 2024: Sakaja asema mlo wa Sh5 kwa wanafunzi Nairobi umeleta tabasamu
GAVANA wa Nairobi, Johnson Sakaja ametaja usambazaji wa mlo wa Sh5 kwa siku kwa kila mwanafunzi kama mojawapo ya sera anazojivunia.
Bw Sakaja amesema mpango huo unaoendeshwa chini ya programu ya Dishi na County, unaendelea kuvutia watoto kujiunga na shule katika gatuzi lake.
Mradi huo wa kaunti, ulizinduliwa Agosti 2023 na mwaka mmoja baadaye, Gavana Sakaja anasema umeandikisha ufanisi.
Alisema umeleta tabasamu kwa watoto wanaotoka familia zisizojiweza kimapato.
Unalenga wanafunzi wa shule za umma za msingi pekee Nairobi.
Aidha, kila mwanafunzi hutoa Sh5 kwa siku.
“Inaridhisha kuona chini ya programu ya Dishi na County kila mwanafunzi anapata chakula cha Sh5 kwa siku,” Sakaja akasema mnamo Alhamisi, Desemba 12 wakati wa maadhimisho ya Jamhuri 2024.
Hafla hiyo ya kitaifa ilifanyika Uhuru Grounds, na iliongozwa na Rais William Ruto.
Bw Sakaja alisema mradi wa Dishi na County umewafaa mamia na maelfu ya watoto, hasa katika mitaa ya mabanda Nairobi ambao kwao kupata chakula huwa kibarua.
Programu hiyo, hata hivyo, imekuwa ikikosolewa, Wakenya wakimtaka Sakaja kutafuta suluhu ya kudumu kwa wenyeji Nairobi.