Wanajeshi 600 wa Somalia walivyotorokea Kenya walipozidiwa vitani Jubbaland
KENYA inahifadhi wanajeshi 600 wa Somalia waliovuka mpaka eneo la Ishiakani kaunti ya Lamu, baada ya kuzidiwa nguvu na wanajeshi wa Jubbaland.
Wanajeshi wa Jeshi la Kitaifa la Somalia walipambana na wenzao wa Jubbaland huko Raaskambooni, mji wa pwani kwenye mpaka wa Kenya na Somalia.
Katika mpaka, wanajeshi wa SNA walisalimisha silaha zao kwa maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) walipokuwa wakitafuta usaidizi.
Waziri wa Usalama wa Ndani Raymond Omollo amethibitisha kuwa Kenya inatarajia kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa SNA Ijumaa.
“Wako Kenya na waliweka silaha chini. Sasa tunashughulikia jinsi ya kuwarudisha katika nchi yao Ijumaa,” alisema.
Awali Dkt Omollo alikuwa ameambia runinga moja ya humu nchini kuwa hali hiyo ni ya kipekee, lakini Kenya inajitahidi kuitatua kwa amani.
Duru zilizo karibu na suala hilo zilisema kuwa wanajeshi hao wa SNA kwa sasa wako chini ya ulinzi wa maafisa wa KDF, wakisaidiwa na Idara ya Kitaifa ya Ujasusi.
“Kinachofanywa kwa sasa ni kwamba tunataka kuhakikisha kuwa hakuna hata mmoja wa askari wa SNA atakayefanikiwa kuingia nchini. Mipango inaendelea kuwarejesha nchini mwao,” afisa mmoja aliyehusika kusuluhisha hali hiyo alisema.
Serikali ya Shirikisho la Somalia (FGS) na Jubbaland zimelaumiana kuhusu nani wa kulaumiwa kwa mapigano hayo.
Maafisa wa Jubbaland walishutumu vikosi vya serikali kwa kuchochea makabiliano hayo ya kivita.
“Vikosi vyetu, katika operesheni zao za ulinzi, vilisababisha hasara kubwa kwa wanamgambo waliosafirishwa kwa ndege kutoka Mogadishu,” Jubbaland ilisema.
Zaidi ya hayo, eneo hili lililo huru lilidai kuwa askari wa Jubbaland walitwaa maeneo ambayo awali yalichukuliwa na vikosi vya shirikisho karibu na Ras Kamboni.
Ras Kamboni iko katika eneo la kimkakati la pwani na inathaminiwa kutokana na ukaribu wake na mpaka wa Kenya na lango muhimu la biashara kando ya Bahari ya Hindi.
Mji huo umekuwa kitovu cha mzozo unaoendelea kati ya FGS na Jubbaland, serikali kuu ikishinikiza udhibiti mkubwa wa majimbo ya kikanda.
Jubbaland inadai kumiliki Ras Kamboni.
Mnamo Somalia ilisema katika taarifa kwamba wanajeshi wa SNA walikuwa wakihakikisha wanalinda watu wao.
“Serikali ya shirikisho ya Somalia, ambayo inatimiza wajibu wake wa kuokoa watu wa Somalia, hasa askari wa Jeshi la Kitaifa walitumwa katika eneo la Juba ya chini kuchukua uthibiti baada ya Atmis kuondoka huko,” taarifa hiyo ilisema kwa sehemu.
Somalia iliongeza kuwa hatua ya kuwatuma maafisa hao ilichochewa na hatua ya Modobe kuchukua kijiji cha Somalia.
Mapigano hayo yanajiri takriban wiki tatu kabla ya muhula kikosi cha kulinda amani cha Muungano wa Afrika kumalizika, bila makubaliano kati ya nchi kuhusu kuendelea kuhudumu , huku kukiwa na changamoto za kifedha.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA