Washukiwa watano wa ubakaji, utekaji nyara walala ndani Kilimani
MAHAKAMA imeamuru wanauma watano wazuiliwe korokoroni kwa muda wa siku tano ili polisi wakamilishe uchunguzi wa madai walihusika na utekaji nyara, ubakaji na kumzuilia mwanamke kinyume cha sheria kwa siku tano.
Patrick Kamau Muthee, Ian Chege, Ismail Mohamed Hamed, Adnan Hussein Jele na Abdirahman Mohammed Ahmed waliamriwa hakimu mwandamizi wa mahakama ya Milimani Bw Gilbert Shikwe wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Kilimani.
Watano hao watarudishwa kortini tena mnamo Desemba 20, 2024 wakati mahakama itafahamishwa na polisi ikiwa wamemaliza kuwahoji na kunakili taarifa kutoka kwa mashahidi.
Bw Shikwe alielezwa na kiongozi wa mashtaka Bi Judy Koech kwamba washukiwa hao walitiwa nguvuni Desemba 11, 2024 na kuzuiliwa katika korokoro ya kituo cha polisi cha Kilimani jijini Nairobi.
Bi Koech alimweleza hakimu kuwa mama yake msichana huyo alifika katika kituo cha polisi cha Kilimani na kusema bintiye alitoweka Desemba 7, 2024.
“Mlalamishi alimsaka bintiye kwa watu wa familia lakini hakufanikiwa. Alifahamisha idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) kisa hicho ndipo uchunguzi ukaanzishwa mara moja,” Bi Koech akasema.
Polisi walifanya kila jitihada na mnamo Desemba 11, 2024 walifanikiwa kumpata msichana huyo akiwa amefungiwa na washukiwa hao katika chumba kimoja eneo la Nairobi West.
Msichana huyo alikutwa amezuiliwa na vijana hao watano wa umri kati ya miaka 21-24.
“Uchunguzi usio wa kina umebaini kwamba msichana huyo alikuwa amebakwa,” Bi Koech alimweleza hakimu.
Walipotiwa nguvuni, washukiwa hao walionekana kama wamebugia pombe kali.
Mahakama iliombwa iruhusu polisi wawazuilie washukiwa hao wakamilishe kuandika taarifa za mashahidi na kupeleka sampuli za DNA kwa Mkemia wa Serikali kuzichunguza.
Mahakama iliombwa ikubalie ombi la polisi.
“Mnapinga ombi hili la upande wa mashtaka kuzuiliwa kwa siku 14 polisi wakamilishe uchunguzi?” Bw Shikwe aliwauliza mashahidi ambao walikubali uamuzi wa kuzuiliwa.
Baada ya kutathmini ombi hilo la upande wa mashtaka, hakimu aliamuru washukiwa wazuiliwe kwa siku tano akisema “siku 14 ni nyingi mno.”
Hakimu aliamuru kesi hiyo itajwe Desemba 20 2024 kwa maagizo zaidi.