Sakaja anavyojikinga chini ya kivuli cha Raila kuelekea 2027
GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja sasa ananingínia kwenye kivuli cha Kinara wa Upinzani Raila Odinga ili kujinusuru na kuwahi muhula wa pili mnamo 2027.
Tangu mfumo wa ugatuzi uanze nchini, hakuna gavana ambaye amewahi uongozi wa Kaunti ya Nairobi kwa mihula miwili.
Aliyekuwa Gavana Evans Kidero alihudumu muhula moja kabla ya kulambishwa sakafu na Mike Mbuvi ‘Sonko’ mnamo 2017.
Bw Mbuvi alihudumu kwa muhula mmoja ila wakati wa uongozi wake Nairobi ilisimamiwa na Shirika la Kusimamia Jiji la Nairobi (NMS) ambalo lilichukua baadhi ya majukumu ya kaunti.
Bw Sakaja, ambaye alichaguliwa kwa tikiti ya UDA 2022, ameonekana kupoteza uungwaji mkono wa wakazi wa Nairobi akilaumiwa kwa utendakazi duni miaka miwili tu baada ya kuchukua usukani.
Aidha Ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti (COB) pia imemweka pabaya akilaumiwa kwa kutoelekeza hata shilingi moja kwenye miradi ya maendeleo.
Katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa kifedha 2024/25, ripoti ya COB iliorodhesha Nairobi kati ya kaunti ambazo hazijaelekeza pesa zozote kwenye miradi ya maendeleo.
Huku nyota ya kisiasa ya Bw Sakaja ikiendelea kudidimia, Gavana huyo ameonekana kuvumbua mbinu ya kushirikiana na Raila akiwa na matumaini kuwa huenda akamsaidia kuchaguliwa tena mnamo 2027.
Bw Sakaja ameonekana kuwa mstari wa mbele kuandamana na Bw Odinga kila mahali huku pia akimminia sifa kigogo huyo wa upinzani sifa kedekede.
Hapa kwa hapa na Raila
Wiki jana, Bw Sakaja alikesha na kulala Addis Ababa akiandamana na Bw Odinga wakati ambapo kiongozi huyo alikuwa ameenda kushiriki Mjadala wa Afrika.
Bw Odinga anawania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Baada ya mjadala huo, gavana huyo alikimbia kwenye mitandao ya kijamii na kudai Raila alishinda mjadala huo.
“Hongera baba. Ujuzi wako kuhuus bara hili, historia na uwezo wake umeonyesha kuwa wewe kweli ni mwana wa Afrika,” akaandika Bw Sakaja kwenye mtandao wake wa X.
Kabla ya ziara ya Addis Ababa, Bw Sakaja pia alikuwa kati ya waliohudhuria sherehe za siku ya kuzaliwa kwa Mama Idah Odinga mnamo Agosti 25, hafla ambayo pia Raila alikwepo.
Wakati ambapo madai yalitanda kuwa madiwani walikuwa wakipanga kuwasilisha hoja ya kumng’oa madarakani mnamo Agosti mwaka huu, inadaiwa gavana huyo alinusurika kutokana na baraka za Raila.
Waziri huyo mkuu wa zamani inadaiwa aliwaagiza madiwani wa Azimio ambao ndio wengi kwenye bunge hilo, wasijihusishe na hoja hiyo.
Aidha Bw Sakaja amefaulu kumuengua Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kwenye kambi ya Raila. Mbunge huyo aliibuka kama mpinzani na mkosoaji wake mkuu na alionekana kama ambaye angemtoa kijasho mnamo 2027.
Bw Owino alijikaanga kwa mafuta yake mwenyewe baada ya kupinga ushirikiano wa Bw Odinga na utawala wa Rais William Ruto.
Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi ambaye alikuwa na umaarufu wa kutwaa uongozi wa kaunti mnamo 2022 kabla ya kuzuiwa kusimama na ODM, naye ameonekana kuwa vuguvugu na hajihusishi sana na kampeni za ugavana.