• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:25 PM
Waislamu wakosoa mbinu ya ugavi wa fedha za kaunti

Waislamu wakosoa mbinu ya ugavi wa fedha za kaunti

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI wa Dini ya Kiislamu wamepinga mtindo mpya uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa mapato nchini (CRA) wa kugawa fedha kwa kaunti wakisema hiyo ni njama ya kuhakikisha kaunti zilizotelekezwa katika tawala zilizopita hazipigi hatua kimaendeleo.

Wakitoa taarifa jana katika Msikiti wa Jamia jijini Nairobi kuhusu masuala yanayokabili taifa, viongozi hao wa mashirika kadhaa ya kutetea haki za Waislamu, walisema kwamba mtindo huo mpya iwapo utakumbatiwa, utazibagua kaunti za KaskazinI Mashariki ambazo wakazi wake wengi ni Waislamu.

“Mtindo wa kuridhisha wa kugawa pesa za ugatuzi unafaa kuhakikisha kwamba maeneo yote yanafaidi. Kaunti zetu zilizotengwa wakati wa serikali zilizopita pia zinafaa kufaidika ili maendeleo yaweze kusambazwa taifa nzima tena kwa usawa,” akasema Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Dini ya Kiislamu(SUPKEM) Yusuf Nzibo.

Wakionekana kuunga mkono wabunge kutoka jamii za wafugaji waliopinga mtindo huo mpya, Bw Nzibo alisema kwamba kuna njama ya kuhakikisha kaunti hizo zinapokezwa kiwango cha chini cha hela kuliko kaunti nyingine nchini na kuzilemaza kimaendeleo.

“Lazima tuhakikishe kwamba maeneo kama Kaskazini Mashariki yanayoendelea kustawi kama maeneo mengine nchini hayatatizwi kimaendeleo. Kabila zote zinafaa kufaidika na rasilimali za nchi kwa kuwa hiyo ndiyo italeta udhabiti wa taifa,” akaongeza Bw Nzibo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati jumuishi ya viongozi wa Waislamu(NAMLEF) Abdullahi Abdi aliwaongoza wenzake kuliunga pendekezo la kuandaliwa kwa kura ya maamuzi na pia kamati ya kuleta uwiano maarufu kama Building Bridges(BBI) iliyobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga.

“Tunaunga mkono kura ya maamuzi ambayo yataongeza fedha zinazopokezwa kaunti na pia kuondoa utawala wa Urais ambao mshindi hutwaa kila kitu na anayeshindwa kusalia bila wadhifa wowote. Tunapigia debe mfumo wa utawala wa bunge kwasababu utasaidia kutuliza joto la kisiasa nchini na kujenga usawa miongoni mwa jamii zote,” akasema Bw Abdi.

Viongozi hao pia walitangaza kuwa watawasilisha mapendekezo yao kwa kamati hiyo a uwianI ili kuhakikisha kwamba matakwa ya Waislamu hayaachwi nje iwapo kura ya maamuzi itaandaliwa.

Bw Abdi vile vile aliomba mabadiliko yafanywe katika Tume huru ya uchaguzi na mipaka(IEBC) ili kuhakikisha kwamba chaguzi zijazo zinakuwa na uwazi na mshindi halali kutangazwa.

Mashirika mengine yaliyowakilishwa ni Baraza la Maimamu na wahuburi nchini, kamati ya Misikiti ya Jamia Shaffi na Njiru kati ya mashirika mengine ya Waislamu.

You can share this post!

SENSA: Walio katika kaunti za mbali waombwa kurejea nyumbani

Wamalwa awataka viongozi waunge mkono vita dhidi ya ufisadi...

adminleo