Polisi walia kunyimwa mamilioni ya huduma zao Eldoret
ZAIDI ya maafisa 600 wa polisi ambao walitoa ulinzi kwa maonyesho ya biashara ya Jumuia ya Afrika Mashariki mjini Eldoret mwishoni mwa mwaka 2018 wanataka kujua zilikoenda zaidi ya shilingi milioni 10 ambazo walipaswa kulipwa kama marupurupu ya kutoa ulinzi.
Kwa mujibu wa mkataba baina ya maafisa hao na wasimimamizi wa maonyesho husika ni kwamba walipaswa kulipwa shilingi 1,800 kwa siku ambapo walitoa ulinzi kwa siku 10.
Maafisa husika ambao hawakutaka majina yao kutajwa kwa kuhofia kuadhibiwa, waliambia wanahabari huenda wakubwa wao wametia pesa hizo mifukoni mwao.
Titus Ominde
“Makataba kati yetu na jumuia ya EAC iliweka wazi kwamba tungelipwa pesa zetu punde tu baada ya maonyesho kukamilika,ni zaidi ya mwezi mmoja tangu pesa hizo zitolewa ili hali hatujalipwa,” alisema afisa mmoja wa polisi
Kwa pomoja maafisa hao walidai kuwa mtindo wa kudhulumiwa na wakubwa wao hasa kwa murupurupu kama hayo umekuwa ukiongezeka kila uchao.
“Kama maafisa tunatakujua ni nani ambaye anakula pesa zetu kila mara, kama sivyo tuondolewe kwa majukumu ya kutoa ulinzi wa kulipwa marupurupu,”alisema afisa mmoja
Kamanda wa polisi katika kaunti ya Uasin Gishu Bw Augustus Nthumbi alikiri kupokea malalamiko kama hayo.
Bw Nthumbi alisema swala hilo lilikuwa nzito kumliko huku akitaka wanahabari kutafuta habari zaidi kutoka kwa kamshna wa kaunti ya Uasin Gishu Bw Abdi Hassan ambaye ni mwenyekiti wa usalama katika kaunti hiyo.
“Siwezi nikasema zaidi kuhusu malalamishi hayo, hata mimi nimeyasikia kama vile nyinyi mmeyasikia, natumai sawala hilo linashughulikiwa na wakubwa wangu,” alisema Bw Nthumbi
Hata hivyo Bw Hassan hakusema lolote kuhusu tetesi hizo kwani hakuwa afisini wana habari walipofika afisini mwake kujua msimamo wake kuhusu swala hilo.